Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam

Yawezekana baadhi ya watu wameshau kwamba kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika zilikuwepo bendi nyingi humu nchini zilizokuwa zikitoa burudani katika sherehe mbalimbali.

Lakini mara baada ya kupatikana kwa Uhuru, kuliundwa bendi iliyopewa jina la NUTA Jazz ambayo kwa sasa ndiyo iliyo kongwe miongoni mwa bendi zilizopo hapa nchini.

Mwaka huu ni miaka 55 tangu ianzishwe mwaka 1964 katika jiji la Dar es Salaam, ikiwa chini ya ummiliki wa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (National Union of Tanzania) kwa kifupi NUTA.

Mwaka huohuo wa 1964 Muhidini Gurumo aliitwa kujiunga na bendi hiyo ya NUTA Jazz akitokea katika bendi ya Rufiji Jazz, na kuwa mmoja wa waasisi wa bendi hiyo.

Gurumo aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama, Mnenge Ramadhani na Wilfred Boniface. Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine zilikuwa Kilimo ni kazi yetu na Mwengele.

Mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri John Simon alijiunga na bendi hiyo ya NUTA Jazz. Mpiga gitaa la solo Amed Omar ndiye liyechaguliwa kuwa kiongozi wa bendi pia ndiye aliyetamba mno katika wimbo wa Mwangele.

Jumuiya hiyo ilipobadili majina kuwa ‘Organization of Tanzania Trade Unions’ kwa kifupi OTTU, bendi nayo ikawa OTTU Jazz. Baada ya kipindi kingine kupita Jumuiya hiyo ikabadili majina kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania, kwa kifupi JUWATA.

Wakati wa uhai wake marehemu Gurumo aliwahi kusema kuwa mpiga solo Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechagualiwa kuwa kiongozi wa NUTA Jazz wakati huo. Mzee Gurumo ambaye ndiye aliye asisi mtindo wa Msondo, ukiwa ni wa asili ya kabila la Kizaramo, aliweza kutamba katika nyimbo.

Baadhi ya nyimbo zilizorekodiwa wakati huo zilikuwa za ‘Baba Nyerere’ , uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine ni ‘Kilimo ni Kazi yetu’ , ‘Mwengele’ , Mpenzi Sofia, Tumeishi toka zamani, na Walinicheka. Zingine zilikuwa Aziza, Tukiwa na Monica shuleni, Sakina, Maneno ya Nyerere, Mipacha Ngui na nyingine nyingi. Wakati huo huo mpiga Solo Saidi Mabera alichaguliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo.

Baadhi ya wanamuziki waliounda Juwata Jazz ni pamoja waimbaji Muhidini Gurumo, Wengine ni Hassan Rehani Bichuka, na mpiga Kinanda Waziri Alli ambaye hivi sasa ni mmoja kati ya viongozi wa bendi ya The Kilimanjaro Band (Wana Njenje).

Waziri kabla ya kujiunga katika bendi hiyo, alikuwa katika bendi ya taarabu ya Lucky Star ya mjini Tanga. Alifika katika jiji la Dar es Salaam akiwa na nia ya kwenda nchini Marekani kujifunza muziki. Juhudi zake hazikufanikiwa akapelekwa na nduguze kwenda kujiunga katika bendi hiyo. Alipotuwa alikabidhiwa kupiga Kinanda.

Miaka hiyo ya 1980 hadi 1990, takribani kila bendi ilikuwa na wapiga vinanda. Ikumbukwe katika bendi ya Maquis du Zaire, alikuwa akibofya Mbuya Makonga ‘Adios’, alikuwepo mwanamama pekee Asia Darwesh aliyekuwa akikipapasa kinanda hususani katika bendi ya MK Group, iliyokuwa ikiga muziki wake katika ukumbi wa Bandari Grill, kwenye hotel ya New Africa, ya jijini Dar es Salaam.

Vijana Jazz walikuwa na Hassan Shaw, ambaye hivi sasa yupo Ughaibuni akipiga muziki katika kumbi mbalimbali za Kitalii. Bima Lee Orchestra walikuwa na Kassimu Magati wakati Abdul Salvador ‘Father Kidevu’ alikuwa akipata ‘ulaji’ ala hiyo.

Ushindani kati ya bendi za muziki wa dansi ulipoongezeka, wanamuziki mwaka 1978 wanamuziki Muhidini Gurumo na Hassan Reheni Bichuka walihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Gurumo alipofika katika bendi hiyo akawa kiongozi wa bendi sanjari na kuasisi mtindo wa ‘Sikinde ngoma ya ukae’. Mtindo huo ambao aliwahi kuelezea ni wa asili ya ngoma za kabila lake la Kizaramo. Baada ya muda mfupi Hassani Bichuka naye aliindoka bendi hiyo Juwata kwenda kuungana na Gurumo katika bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Baada ya Bichuka kupondoka, uongozi ukamchukuwa mwimbaji aliyekuwa akishabihiana naye kwa sauti, Shaaban ‘Kamchape’ akitokea katika bendi ya Dodoma International ya mjini Dodoma.

Gurumo alirejea tena katika bendi yake ya Juwata mwaka 1991, akapewa wadhifa wa kuwa kiongozi wa bendi hiyo, baada ya kupiga muziki katika bendi hiyo ya Mliamani Park Orchestra pamoja na Orchestra Safari Sound (OSS) kwa nyakati tofauti.

Nyimbo walizotoka nazo zilikuwa za Nidhamu ya kazi, Ete, Queen Kasse, Mariamu ninakujibu, Usia wa baba, Msafiri kafiri, Tupa tupa, Ndugu Kassimu na nyingine lukuki.

Baadaye bendi hiyo ilibadilishwa jina na kuwa OTTU Jazz kufuatia kubadilika kwa jina la Chama cha Wafanyakazi kuwa OTTU. Hakuna ubishi kwamba bendi ya OTTU Jazz au kwa jina lingine wakajiita ‘Baba ya Muziki’, ilitikisa jiji la Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla wakipigia kwa mtindo wa wa ‘Msondo Ngoma, magoma Kitakita’ au ‘Mambo hadharani’.

Wakati huo ilikuwa katikati ya wimbo wapenzi na mashabiki wa Msondo walikuwa wakiimbishwa kibwagizo cha “Msondo yee Msondo Waa…” wapenzi na walikuwa wakiitikia “Afyaaaa”. Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Amana uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, ikipakana na hospitali ya Amana.

Katika kipindi hicho bendi hiyo ilikuwa imesheheni wengi wenye vipaji vinavyotofautiana. Wanamuziki hao walikuwa akina Joseph Lusungu, Mnenge Ramadhani, Muhiddin Maalim, Hassan Rehani Bitchuka, Saidi Mabera na TX Moshi William. Wengine ni pamoja na

Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustapha John Ngosha, Suleimani Mwanyiro ‘Computer’, Tino Maselenge (Masinge) ‘Arawa’ Abdull Ridhiwan Pangamawe, Roman Mng’ande ‘Romario’ na Athumani Momba. Wengine ni Salehe Bangwe ‘Mwana Kigoma’, na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na Said Mabera mpiga solo mahiri ambaye tangia ajiunge katika bendi hiyo hajathubutu kuiondoka.

Kufuatia Hospitali ya Ilala kupanuka, OTTU Jazz walitakiwa kuondoka kwa kile kilichodaiwa ni kuwabughudhi wagonjwa kwa makelele ya vyombo vya muziki wao. Hivyo walilazimika kuhamia katika ukumbi wa AfriCenter uliopo barabara ya Kigogo, ambako nako hawakudumu kipindi kirefu na hivi sasa wanapiga muziki wao popote wanapoalikwa hususan wamiliki wa Baa, ambapo huwa hakuna kiingilio ili kununua kinywaji chako.

Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’ na OTTU Jazz zilikuwa za Kicheko, Mawifi mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama katika dimbwi, Mti mkavu na Mizimu. Zingine ni Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la mlemavu, Piga ua talaka utatoa, Tuma, Wapambe, Asha mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya kusikitisha, Mwana mkiwa, Kalunde, Kaza moyo, Jesca, Kwenye penzi, Binti maringo, Dalili na nyingine nyingi.

Chama cha Wafanyakazi Tanzania baadaye kijiondoa katika ufadhili wa bendi hiyo, kikawaachia vyombo wajitegemee. Walijikusanya kutengeneza mikakati na kuamua kuipa jina la bendi kuwa Msondo Ngoma ikiwa imesheheni wanamuziki wengi wakiwemo wa zamani na wapya.

Msondo Ngoma ina jumla ya wanamuziki 18 na fundi mitambo mmoja. Kiongozi wao ni Said Mabera ambaye pia ni mpigaji wa gita la Solo. Waimbaji wa bendi hiyo ni akaina Juma Katundu, Fresh Jumbe, Shaaban Dede, Twaha Mohamed, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.

Wakung’utaji magita ni akina Abdull Ridhiwani Pangamawe ambaye ni bingwa wa kupiga kinanda, Solo na Rhythm, Huruka Uvuruge naye pia ni mpigaji wa Solo na Rhythm, Kassimu Mponda, Mustafa Hamis ‘Pishuu’ na Zahoro Bange wakicharaza gitaa la rhythm.

Kwa upande wa gita zito la besi wapo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’. Drums huchanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe.

Tarumbeta hupulizwa na kijana machachari Roman Mng’ande ‘Romari’ na Hamis Mnyupe. Dorice George hupiga Tumba, Drums ambaye pia ni Mwimbaji wakati Amiri Said Dongo naye ni mpigaji wa Tumba. Mtunzi na mwimbaji mahiri Shabani Dede ‘Kamchape’ alirejea tena katika bendi hiyo akitokea bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde’.

Talanta za kutunga na kuimba za marehemu TX Moshi William, ambaye inasemekana yeye ndiye alikuwa mtunzi mkuu katika bendi hiyo. Inaaminika kuwa katika albamu moja waliokuwa wakiifyatua, TX alikuwa katunga nyimbo 8 hadi 9 wakati zilizobaki zinatungwa na Jumuiya.

Tofauti kabisa na miaka ya nyuma upinzani kati ya bendi za Mlimani Park na Msondo Ngoma Classic uliokuwa ukishihudiwa nyakati zile, umepungua kwa kiasi kikubwa. Bendi hizo hufikia kuandaa siku ya kupiga muziki kwa pamoja katika viwanja vya TTC Chang’ombe, jijini Dar es Salaam.

Bendi ya Msondo Ngoma Classic bado ipo ikiwa na makao yake katika baa ya Dimax iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wanamuziki wanaotajwa katika makala hii wamekwisha tangulia mbele za mungu akiwemo Mzee Muhidini Gurumo.

Wengine ni TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Hamis Kitambi, Mustafa John Ngosha, Suleiman Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’, Athuman Momba na wapulizaji wa saxophone Mnenge Ramadhani na Alli Rashidi aliyefariki dunia siku ambayo bendi hiyo ikitimiza miaka 50, Oktoba 10, 2014.

Mungu azipumzishe roho zao pahala pema peoni, Amina.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba:
0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...