Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela akitazama makazi ya wananchi wa Mtaa wa Shule ulioko jirani na Shule ya Msingi Mlowo, Wilayani Mbozi ambapo takataka zimemwaga katikati ya makazi ya wananchi kabla ya kuagiza kufungwa kwa dampo hilo.
Wananchi wa Mtaa wa Shule wakitazama takataka zilizomwagwa jirani na makazi yao mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela kupita mtaani hapo na kuagiza dampo hilo lifungwe.

……………………

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela ameagiza kushikiliwa na polisi kwa masaa 24 Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo Seriadi Mbugi kutokana na kurundika takataka jirani na makazi ya wananchi pamoja na shule ya Msingi Mlowo na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amefikia uamuzi huo mapema leo wakati akifanya ukaguzi wa hali ya usafi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo na kukuta takataka zimemwagwa katikati ya makazi ya wananchi ikiwa ni siku saba tangu amuelekeze Kaimu Mkurugenzi huyo kuhakikisha mji huo unakuwa Msafi.

“Nilifanya Mkutano na wananchi wa Mji wa Mlowo na malalamiko yao makubwa yalikuwa mrundikano wa takataka na madampo katikati ya miji yao, nilimuagiza na kumpa siku saba Mkurugenzi wa Mji mdogo wa Mlowo kuhakikisha anausafisha mji huu lakini leo siku saba zimepita ninakagua na kukuta takataka zimemwaga katikati ya makazi ya watu, naambiwa watoto wanacheza na kuokota taka hapa, huu sio ubinadamu”, amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela

Ameongeza kuwa Mkurugenzi huyo amekiuka agizo lake na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi hao kwa kuwawekea takakata wananchi katikati ya makazi yao kinyume na taratibu za kiafya zinavyoelekeza.

“Huu sio utendaji wa serikali kabisa, licha ya Kaimu Mkurugenzi wa Mji Mdogo kukaa ndani, namuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuhakikisha ndani ya masaa manne takataka hizo ziwe zimetolewa na dampo hilo lifutwe”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela

Kwa upande wake mkazi wa mtaa wa shule Bi Salehemu Filimon Mwaihojo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea eneo hilo na kutatua kero hiyo kwakuwa wamekuwa wakipata hofu ya magonjwa kutokana na uwepo wa takataka hizo

“Hii ni wiki ya pili wanamwaga matakataka hapa, watoto wanachezea na kuokota makopo wanachota maji machafu na kunywa kwenye makopo hayo machafu wengine unakuta wanaokota kondomu zinazomwaga hapa wanapuliza wao wanajua mipira, kwakweli tulikuwa na hali mbaya, kwakuwa tuliona wametumwagia magonjwa hapa”, amesema Mwaihojo

Ameongeza kuwa dampo hilo lipo pia jirani na Shule ya Msingi Mlowo na hivyo wanafunzi hupita na kuchezea hapo hali ambayo wangeweza kudhuriwa na vipande vya chupa na taka ngumu zinazo mwagwa hapo huku wengine wakiokota na kula mabaki ya vyakula yanayotupwa hapo na hivyo kuhatarisha afya zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...