Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika ‘The Pan African Parliament Bureau’ imekutana na Mabalozi ‘Ambassadors’ wanaowakilisha mataifa mbalimbali barani Afrika katika nchi ya Afrika Kusini kujadili masuala kadha wa kadha kuhusu bara la Afrika. 
Mkutano huo ukiongozwa na Rais wa Bunge la Afrika,Mheshimiwa Roger Nkodo Dang kutoka Cameroon, umefanyika leo Ijumaa Mei 3,2019 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Bunge la Afrika kama sehemu ya mkutano wa maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Bunge la Tano la Bunge la Afrika jijini Johannesburg Afrika Kusini.
Akizungumza wakati wa mkutano huo wa Mabalozi wa Afrika walioidhinishwa na Jamhuri ya Afrika Kusini, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele ambaye ni mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini na Naibu Waziri wa zamani nchini Tanzania alisema Bunge la Afrika litajadiliana na kutoa Azimio juu ya tabia ya Xenophobic nchini Afrika Kusini.
“Suala hili linapaswa kuchukuliwa kwa umakini, kuna vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na vikundi tofauti kutoka nje inaonekana kama Afrika Kusini haitaki wageni katika nchi yao… La hasha lakini kwa undani kuna matendo ya uharifu kwa kivuli cha Xenophobia”,alisema Mhe. Masele. 
“Ninafurahi na kuhamasishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini ili kukabiliana na mambo yote ya uhalifu.Tutakuwa makini sana wakati tunajadiliana jambo hili kwa sababu hatutaki kuingilia kati mambo ya ndani ya Afrika Kusini au kuingilia kati vyombo vya usalama kutekeleza majukumu yao”,aliongeza.
Masele aliomba mamlaka ya Afrika Kusini kushughulikia suala la tabia ya Xenophobic katika Afrika kwani haikubaliki.
“Sisi kama Wabunge wa Afrika tunatarajia kuona hatua kali zikichukuliwa dhidi ya waharifu wote, wanaharibu sifa nzuri ya Afrika Kusini na Afrika. Bunge la Afrika litapaza sauti na kukemea suala hili..Vikwazo vya hali yoyote dhidi ya watu binafsi au nchi huumiza watu wasiokuwa na hatia hususani wanawake na watoto na huzuia jitihada za maendeleo za watu wetu na nchi ambazo zina vikwazo”,aliongeza.
Kikao cha Pili cha kawaida cha Bunge la Tano la Afrika kinatarajiwa kuanza mnamo Mei 6, 2019 huko Midrand - jijini Johannesburg Afrika Kusini.
Pamoja na mambo mengine , watajadiliana juu ya Kauli mbiu ya Umoja wa Afrika ya mwaka huu "Mwaka wa Wakimbizi na Watu Waliopotea",ambapo pia Bunge la Afrika litajadili Suluhisho la Kudumu juu ya tatizo la wakimbizi barani Afrika.
Hali kadhalika Bunge hilo, litajadili taarifa juu ya amani na usalama katika bara la Afrika ikiwa ni pamoja na maendeleo ya hivi karibuni na hali ya kisiasa Libya, Sudan, Algeria na mchakato wa amani nchini Sudan Kusini. 
Masele anahimiza pande zote zinazohusika katika majadiliano ya amani zisiwe na upendeleo kwa lengo la kutimiza ahadi zilizotolewa kwa watu wa Afrika. Angalia picha za matukio wakati wa mkutano Wajumbe wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika na Mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali barani Afrika katika nchi ya Afrika Kusini wakiwa kwenye mkutano leo Ijumaa Mei 3,2019 jijini Johanesburg Afrika Kusini. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Makao Makuu ya Bunge la Afrika,Midrand,Johanesburg,Afrika Kusini. Rais wa Bunge la Afrika,Mheshimiwa Roger Nkodo Dang kutoka nchi ya Cameroon akizungumza wakati wa mkutano wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika na Mabalozi wa nchi za Afrika nchini Afrika Kusini. Kulia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele akiandika dondoo muhimu wakati wa mkutano wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika na Mabalozi wa nchi za Afrika nchini Afrika Kusini. Wajumbe wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika na Mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali barani Afrika katika nchi ya Afrika Kusini wakiendelea na mkutano. Wajumbe wa Kamati ya uongozi ya Bunge la Afrika na Mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali barani Afrika katika nchi ya Afrika Kusini wakiwa wamesimama kuwakumbuka watu waliofariki dunia kutokana na majanga yaliyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika yakiwemo mafuriko na Kimbunga Keneth. Mkutano ukiendelea. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...