Na Karama Kenyunko, globu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya dola za Marekani milioni 112 dhidi ya aliyekuwa rais wa Migodi ya Pangea, North Mara, exploration na Bulyanhulu, Deogratius Mwanyika na wenzake waeleze upelelezi wa kesi hiyo, umefikia hatua gani.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina amesema hayo leo Mei 17,2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili  ya kutajwa na Wakili wa Serikali Wankyo Simon kudai upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika wanasubiri taarifa kutoka nje ya nchi ambako wameomba msaada.

Kutokana na taarifa hiyo, Wakili Wa utetezi Nyika  ameomba upande wa mashtaka waeleze bado muda gani upelelezi huo utakamilika kwani mara kwa mara wamekuwa wakisema upelezi bado kuna maeneo bado hawajakamilisha lakini hawasemo ni maeneo gani.

Hata hivyo baada ya maelezo hayo kutolewa  Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, mwaka huu na ameutaka upande wa mashtaka siku hiyo kueleza upelelezi umefikia hatua gani
Mbali na Mwanyika washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu Alex Lugendo,  Mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku Assa Mwaipopo,kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.Wanakabiliwa na tuhuma za mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya dola za Marekani milioni 112.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama , mashtaka saba ya kughushi , mashtaka 17 ya Utakatishaji wa fedha, Kuwasilisha nyaraka  za uongo  kwa  Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA), shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka nane ya kukwepa kodi na shtaka moja la kutoa Rushwa.

Wanadaiwa, kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30,2007 katika sehemu tofauti za jiji la dar es Salaam, Kahama Mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera maeneo ambayo yapo katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na nchini  Uingereza.
Aidha mshtakiwa Mwanyika  na Lugendo, wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa kamishna Generali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya dola 9,309,600 ambayo ilikuwa ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Pia Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha kiasi cha dola 374,243,943,45 huku wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Wanadaiwa kati ya Novemba 2,  2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa rushwa ya Sh. 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai waligushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea limited ilikubali kukopa dola za Marekani 90,000,000 ikiwa na riba kutoka benki ya kimataifa ya barrick huku wakijua kuwa siyo kweli.

Wakati katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018 huko BOT iliyopo wilaya ya ilala, kwa makusudi aliwasilisha  nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni mgodi wa Bulyanhulu na Barrick international bank Corp kwa madhumuni ya kuonesha kuwa, kati ya June 2001 na Desemba 13, 2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa dola za Marekani 416,100,000 kutoka Barrick.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...