Na Karama Kenyunko,Michuzi TV
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia mashtaka mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) Robert Kisena (46) na mkewe Frolencia Mashauri nisha kukamatwa tena na kuunganishwa katika kesi moja yenye  mashitaka 19 ikiwemo kusababisha hasara kwa UDART ya Bil.2.41.

Awali washtakiwa hao  walikuwa wakishtakiwa  pamoja na wenzao watatu mbele ya Mahakimu Thomas Simba na Augustine. Mbali na Kisena na Mkewe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena(33), Charles Newe(47) na raia wa China, Cheni Shi (32).

Baada ya kufutiwa mashitaka yao chini ya kifungu namba 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 walikamatwa na kuunganishwa katika kesi moja.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire  Wakili wa Serikali, Grory Mwenda amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka 19 likiwemo la  Kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, Wizi wa mafuta, utakatishaji fedha wa Bil.1.2, kughushi na kusababisha hasara ya Bil.1.4.

Katika kosa la utakatishaji fedha linamkabili Robert Kisena na Chen Shi inadaiwa Aprili 8,  2016 katika benki ya NMB Kisena akiwa Mkurugenzi wa UDART alihamisha Sh.Mil 594.92 kwenda kwenye akaunti nyingine ya Kampuni ya Longway Engineering Company wakati akijua fedha hizo ni zao haramu lililotokana na makosa ya kughushi.

Pia  washitakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na December 2016 wakiwa Dar es Salaam waliisababishia hasara UDART  ya Bil.2.41.

Aidha katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu linalomkabili Kisena na Shi imedaiwa June 9, 2016 katika tawi la NMB Ilala washtakiwa kwa nia ya  ovu waijipatia Mil.603.25 kutoka UDART kwa kuonyesha kiwango hicho kimelipwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa  Kituo cha UDART Kimara, Ferry  (Kivukoni), Ubungo na Morocco.

Hata hivyo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Mei 28, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...