Mwandishi Phelisters Wegesa Marwa

Nyumbani kwetu Tanzania ni mbali na Jamhuri ya Watu wa China, lakini kutokana na urafiki mwema na wa muda mrefu kati ya China na Tanzania, nimeweza kuishi na kusoma katika taifa hili kama ambavyo ingekuwa nikiwa nyumbani Tanzania. 

Mnamo mwaka 2016 mwezi Agosti nilifunga mizigo yangu na kusafiri angani takriban maili 5,340 kutoka Dar es Salaam, mji wa kibiashara wa Tanzania hadi Beijing nchini China kwa ajili ya kuongeza maarifa katika fani yangu.
Katika kipindi cha nyuma kabla sijafika katika Taifa hili la China, niliweza kufanya ziara katika Nchi mbalimbali za Afrika na hata Ulaya/Amerika kwa ajili kuhudhuria vikao, semina, mafunzo ya muda mfupi na makongamano ambapo nilikaa wiki au miezi michache katika Nchi hizo. Tofauti na Nchi zinazozungumza Kiingereza na Kiswahili lugha kuu ya mawasiliano katika shughuli mbalimbali za kila siku Nchini China ni lugha ya Kichina. 

Uamuzi wa Mimi kuja kusoma katika taifa hili uligubikwa na mawazo kinzani kutoka kwa baadhi ya watu wenye dhana kuwa mtu yeyote anayekwenda China ni kwa sababu ya kufanya biashara na sio kusoma: Lakini kwangu mimi sikuipa nafasi dhana hiyo bali niliendelea kusisitiza juu ya uamuzi wangu wa kuja China kwa ajili ya masomo na kuongeza maarifa mengine katika fani yangu.

Uamuzi wangu wa kusoma na kujifunza nje ya nchi na hasa China ni kutokana na sababu kwamba kuna mengi zaidi ya kujifunza duniani na hasa mataifa mengine zaidi ya Marekani ukizingatia kuwa Taifa hili la China ni taifa la pili baada ya Marekani kwa ukubwa wa Uchumi wake.

Kutokana na Imani yangu hiyo niliweza kutuma maombi ya kupatiwa udhamini wa masoma ambapo Ofisi ya Uchumi na Biashara ya Ubalozi wa China nchini Tanzania iliweza kunichagua kuwa miongoni mwa watakaopewa udhamini wa masomo Nchini China kwa ufadhili wa Wizara ya Biashara ya Jamhuri ya Watu wa China (MOFCOM)katika Chuo Kikuu cha Beijing ambacho kwa sasa pia ni Taasisi ya Utafiti wa mpango wa Rais wa China XI JIN PING ujulikanao kama “Belt and Road”. 

Mwaka 2019 ni kumbukizi ya miaka 55 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya China na Tanzania; Mataifa haya yana ndoto ya pamoja. Ndoto ya ushirikiano wa kiuchumi na ushirikiano wa maendeleo ya pamoja katika nyanja mbalimbali, ndoto hii na ushirikiano kati ya China na Tanzania imeasisiwa miaka mingi iliyopita wakati hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere walipokutana na Mwenyekiti hayati Mao Zedong na michakato mbalimbali ya safari ya kutimiza ndoto hizi ulipoanza.

Historia ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA),ni mradi mkubwa zaidi wa msaada wa kigeni nchini Tanzania na Afrika, hadi sasa kuna uwekezaji mwingine unaoungwa mkono na serikali ya watu wa China kama vile Kiwanda cha kutengeneza nguo cha Urafiki, Shamba la mpunga la Mbarali, Mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, Kiwanda cha miwa cha Mahonda, Uwanja wa Taifa wa mpira wa Miguu, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Maktaba ya Kimataifa ya sanaa ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam, mradi wa ujenziwa bandari ya Bagamoyo pamoja na mtandao wa reli unaounganishwa na reli nyingine za Tanzania. Historia hii ina maana kubwa sana katika uhusiano kati ya China na Tanzania na hata Afrika kwa ujumla.
Mwenyekiti wa muda mrefu China, Mao Zedong pamoja na Rais wa kwanza wa Tanzania, J. K. Nyerere, Machi 25, 1974.

China na Tanzania wanaendelea kuimarisha ushirikiano wa kisiasa kwa njia ya ziara za mara kwa mara za viongozi wa serikali za nchi hizi mbili. Rais wa wa sasa wa China Xi Jin Ping alichagua Tanzania kuwa kituo chake kwanza cha ziara yake ya Afrika mwaka 2013 baada ya kuchukua madaraka na hii inathibitisha umuhimu wa mahusiano ya China na Tanzania. 

Aidha, kumekuwa na ziara zingine za kukuza mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili ikiwa ni uzinduzi wa miradi mbalimbali kama vile Elimu, Miundombinu, Afya, Utalii, Mbinu za Kilimo za Kisasa, Mauzo ya Nje na Uagizaji ambayo umeimarisha uhusiano zaidi na kubadilishana uzoefu. 

Rais wa China Xi Jin Ping (Kulia) na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kwenye mkutano wa China-Afrika Forum(FOCAC) Septemba3-6, 2019 uliofanyika katika Mji Mkuu- Beijing, China.

Tanzania imejihusisha kushiriki kikamilifu katika Mpango wa Belt and Road ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alihudhuria kwenye Mkutano wa Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) ambapo aliweza kuwa na mazungumzo ya pande mbili(bilateral) na Rais Xi Jin Ping na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wenye manufaa kati ya pande zote mbili. China imepongeza juhudi za Tanzania katika kulinda haki na maslahi ya watu wake, kuendeleza uchumi wa Viwanda na kuboresha maisha ya watu, na iko tayari kuimarisha na kubadilishana uzoefu wa utawala, maendeleo na mikakati ya kupunguza umaskini.

Taifa la China kinara duniani katika kupunguza umaskini hivyo kuna mengi ya kujifunza kutokana na uzoefu wake. China inachukua jukumu zaidi katika ngazi ya kimataifa kutokana na kuwa taifa lenye Uchumi Mkubwa duniani baada ya Marekani naTanzania ina nafasi nzuri ya kuendelea kushirikiana na kujifunza kutoka China na kufanya kazi pamoja kuwekeza nguvu zake zaidi katika viwanda na uvumbuzi.

Wizara ya Afya na wadau muhimu kutoka Tanzania na China wamekutana mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Afya kwa njia ya miradi ambayo tayari imeanzishwa. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ndio taasisi ya moyo ya kwanza nchini Tanzania ambayo tangu kuanzishwa kwake Oktoba 2015, taasisi hii ya JKCI imefanikiwa kutibu maelfu ya wagonjwa wa moyo na kufanya upasuaji wa moyo zaidi ya watu 1,500 kwa gharama nafuu, na hivyo kuleta faida kubwa kwa watanzania. 

Hivi sasa, kuna madaktari watatu wa kichina wanaofanya kazi katika taasisi hii ya JKCI waliobobea katika upasuaji wa moyo na magonjwa ya watoto. Hivi karibuni taasisi hiiya JKCI imesaini mkataba wa makubaliano na Hospitali ya Fuwai iliyopo nchini China ambayo ni kituo kikubwa kinachoshughulikia matatizo ya moyo na hospitali hii ya Fuwai ina umaarufu sana duniani katika matibabu sugu ya aina tofauti ya moyo.
China imeonyesha kujitolea kwa kupanua upatikanaji wa huduma za afya, kuanzia Mfumo wa Matibabu wa Ushirika,upatikanaji wa ubora wa huduma za afya ambayo imekuwa mojawapo ya eneo la kimkakati na linalotiwa msisitizo na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China pamoja na Wizara ya Afya ya Tanzania na pia kuna miradi ya pamoja na mafunzo ya wataalam na ushirikiano wa taasisi za afya za Nchi hizi mbili.

Waziri wa Afya wa Tanzania Mheshimiwa Ummy Mwalimu alikutana na kufanya Mazungumzo na Waziri wa Afya wa China Ma Xiaowei walikubaliana kuwa China itaendelea kupeleka timu ya wataalamu wa afya pamoja na matibabu Tanzania ili kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika matibabu ya angiocardiopathy, kansa, afya ya umma, pamoja na mafunzo ya madaktari wa kitaaluma na ujanibishaji wa bidhaa za dawa. Ziara hii Ilihitimishwa kwa kusaini mkataba wa ushirika kati ya Hospitali ya Saratani ya Kichina ya Sayansi ya Matibabu ya China na Taasisi ya Saratani Ocean Road Tanzania.
Waziri wa Afya MheshimiwaMhe. Ummy Mwalimu pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki na wataalamu wengine wa afya kutoka China na Tanzania wakati wa ziara katika Hospitali ya Kimataifa ya Peking University (PUIH). 

Watanzania wana kila sababu ya kudumisha uhusiano wa China na Tanzania na mustakabali wa mahusiano haya yapo mikononi mwa vijana wote waliopata nafasi ya kuja kujifunza nchini China na pia wale walio Tanzania kujifunza kwa wachina waliopo Nchini Tanzania. Ni jukumu la vijana kufanya na kuonyesha umahiri katika yale tuliyojifunza katika taifa hili la China, Elimu hii iwe ni funguo katika kukuza maendeleo mapya na mafanikio ya nchi ya Tanzania na China. 

Hii itasaidia kuongeza kasi ya mageuzi na mabadiliko yaliyopangwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt John Joseph Magufuli. Hivyo China kama mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania, Tanzania inahitaji China katika mkakati wa viwanda ili iweze kufikia lengo la kuwa na uchumi wa katiifikapo mwaka 2025 kwa kuzingatia agenda ya Nchi yetu ya Mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji. 

Mustakabali wa kesho wa Nchi yetu unaonekana kuwa mzuri na wenye mafanikio, tukiweza kudumisha na kuenzi ushirikiano wa elimu ya juu sayansi na teknolojia pamoja na utafiti ni suluhisho muhimu kuimarisha uchumi wetu na Tanzania ya Viwanda. 

Ni imani yangu kwamba msingi wa urafiki uliojengwa kati ya China na Tanzania utafikia kizazi cha baadaye kwa kufanya kazi pamoja ili kujenga jumuiya yenye nguvu zaidi kwa manufaa ya watu wa Nchi hizi mbili, Afrika na hata dunia kwa ujumla. 


Udumu Urafiki wa China na Tanzania! 

Phelisters Wegesa Marwa 

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Tanzania ambaye pia ni Mwandishi wa kujitegemea wa makala ya Uchumi, Vijana, Elimu na Ushirikiano wa China na Afrika. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...