Na Karama Kenyunko, globu ya jamii

MFANYABIASHARA wa mafuta ambaye ni raia wa Somalia anayeishi jijini Nairobi nchini Kenya, Abshir Afrah (56), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na tuhuma za mashitaka matatu likiwemo shtaka la kukwepa kodi ya Sh. bilioni 8.1.

Akisoma mashitaka, leo Mei 22, 2019, Wakili wa Serikali Wankyo Simon amedai, mshitakiwa anakabiliwa na tuhuma za kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka matatu ambayo ni kukwepa kodi, kuisababishia TRA hasara na utakatishaji wa fedha.

Imedaiwa, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega kiwa, kati ya mwaka 2015 na 2018 ndani ya jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa Afrah alikwepa kodi ya kusambaza mafuta ya Sh 8,107,509,385.48 kinyume na sheria ya kodi ya mwaka 2015.

Pia imedaiwa kati ya 2015 na 2018 maeneo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jijini Dar es Salaam, kinyume na sheria mshtakiwa aliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. bilioni 8.1 kwa kukwepa kulipa kodi.

Aidha siku na mahali hapo mshtakiwa huyo alitakatisha fedha na kujipatia Sh.bilioni 8.1 kwa kukwepa kulipa kodi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu wa kosa la kukwepa kodi akiwa na nia ya kuficha ukweli wa fedha hizo

Hata hivyo, mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo waliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 4, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana.


MFANYABIASHARA wa mafuta,raia wa Somalia anayeishi jijini Nairobi nchini Kenya, Abshir Afrah (56),  akitoka katika chumba cha  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  baada ya kusomewa  mashitaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili ambapo mashtaka hayo ni kukwepa Kodi, kuisababishia TRA hasara na utakatishaji wa fedha zaidi ya sh. Bil, 8.1

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...