*Asema mashirika yasiyotoa gawio yahakikishe yanatoa kabla ya kumalizika kwa Julai

*Asema watakaoshindwa kuchukuliwa hatua , atoa maagizo kwa ofisi za umma

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

RAIS Dk.John Magufuli ameagiza mashirika yote 253 yaliyopo nchini ambayo Serikali ina hisa yawe yametoa gawio kabla ya kumaliza Julai mwaka huu huku akisisitiza wote ambao hawajatoa waandikiwe barua kwani ni lazima waliopewa jukumu watimize wajibu wao.

Amesema haiwezekani mashirika 24 tu ndio yawe yametoa gawio la Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 huku akisisitiza mashirika kutoa gawio kwa Serikali fedha hizo ndizo ambazo zinatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo nchini ikiwemo ya ujenzi wa kituo vya afya pamoja na miundombinu mingine.

Rais Magufuli amesema hayo leo Mei 21,2019 wakati Shirika la Simu Tanzania(TTCL) likitoa gawio kwa Serikali ambapo limekabidhi gawio la Sh.Bilioni 2.1.

"Nipowapongeze TTCL kwa namna ambavyo mmekuwa mstari katika kutoa gawio kwa Serikali.Ni uzalendo huu ambao mmeuonesha na naamini mwakani tarehe kama ya leo mtanialika tena kuchukua gawio la Serikali," amesema Rais Dk.John Magufuli.

Wakati huo huo ,Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kutoa maagizo kwa mashirika yote ambavyo hajatoa gawio la Serikali kutoa gawio kabla ya kumalizika Julai mwaka huu na kumtaka Msajili wa Hazina kuyaandikia barua mashirika hayo na kufafanua kati ya mashirika hayo ni 24 tu ndio yamelipa gawio.

Rais Magufuli amesema mashirika yatoe gawio na lazima yabanwe kwani kutoa gawio ni takwa la kisheria huku akisisitiza haiwezekani mashirika yasitoe gawio kwa kisingizo cha kutopata faida.

"Ni lazima yatoe gawio na kabla mwezi huu kwisha nipate majina ya mashirika ambavyo yatakuwa hajatoa ,kama hayapati faida kwanini wanaendelea kuwepo na hata namna ambavyo waliyapata mashirika ni sasa na bure," amesema.

Wakati huo huo Rais Magufuli amesema amesikitishwa na taarifa ya ofisi nyingi za Serikali kutotumia mawasiliano ya simu ya TTCL licha ya kwamba yeye mwenyewe alitoa maagizo mwaka jana.

Amesema amesikitika zaidi baada ya kusikia hata Ofisi ya Rais Ikulu nayo haikutajwa na TTCL kuwa miongoni kwa wanaotumia mawasiliano hayo. Ameagiza ofisi za Serikali zote ikiwemo ofisi yake kuhakikisha zinatumia laini za TTCL na kwamba yeye anayo laini ya TTCL ambavyo anailipia kwa fedha zake mwenyewe.

Amesisitiza wakuu wa idara pamoja na watumishi wengine wa Serikali kuhakikisha wanakuwa na laini za TTCL na kwamba amemwambia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Waziri Waziri Kindamba kumuandalia orodha ya wakurugenzi ambao wanatumia laini za shirika hilo.

"Nataka uniandikie majina ya wakurugenzi ambao wanatumia laini za TTCL na sio kwamba wanazo tu nataka nione zinatumika.Sio kwamba msiwe na laini za kampuni nyingine hapan,Ila nataka hizi ambazo Serikali inatoa fedha kwa ajili ya mawasiliano basi ziende kwa shirika hili ambao ni la kwetu Watanzania na lazima tulijengee uwezo ili lijiendeshe," amesema Rais Magufuli.

Pia ametumia nafasi hiyo kuzungumzia fedha ambazo Shirika hilo inalipa kwa ajili ya kulipia minara  ambapo amesema umefika wakati kuwa na minara yake kwani haoni sababu ya kuendelea kuona TTCL inatumia fedha nyingi kulipia gharama ya minara ya simu.

Awali Waziri Kindamba ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ambayo Shirika la TTCL wameyapaya bado wanahitaji fedha zaidi kujiendesha na hivyo amekumbusha kupatiwa fedha ambazo Serikali iliahidi ambapo Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Fedha kutoa fedha hizo kwa shirika hilo.

Ameongeza kuwa gawio la Sh.bilioni 2.1 ambalo wamelitoa kwa Serikali inatokana na kazi  nzuri ambayo inafanywa na wahasibu wao katika kuandaa hesabu na kisha kupitiwa na mkaguzi wa ndani na baada ya hapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Amesema kutolewa kwa gawio hilo ni baada ya kupitiwa kwa hesabu na kisha faida ambayo wameipata sehemu ya fedha ndio hilo gawio ambalo ni ongezeko la Sh.milioni 600 ukilinganisha na mwaka jana.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Gawio la Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 2.1 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Waziri Kindamba, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Omar Nundu katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...