Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.




Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Dodoma

Serikali iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji kwa lengo la kubaini ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za mradi na mahitaji halisi ya sasa ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi mipya ya umwagiliaji.

Aidha, baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa umwagiliaji katika bonde la Mkomazi zinaendelezwa na kuwanufaisha wananchi wa Mombo na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 16 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Mhe Timotheo Mnzava aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali katika utekelezaji wa mradi wa Umwagiliaji katika Bonde la mto Mkomazi.

Alisema kuwa katika miaka ya 1980 Serikali kupitia washirika wa maendeleo, Wakala wa Ushirikiano wa Kitalaam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany Agency for Technical Cooperation Ltd) ulifanya upembuzi yakinifu (Feasibility studies) kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi katika tarafa ya Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa za upembuzi yakinifu na usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ungesababisha kuongezeka kwa maji katika ziwa Manga na kupelekea kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na mashamba ya wakulima.

Mhe Mgumba alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo katika mwaka 2014/2015, wataalam wa ofisi ya kanda ya umwagiliaji ya Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu uliofanywa katika eneo hilo kwa lengo kuepusha uwezekano wa kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni na Mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa. Mapitio hayo yalibaini uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiliaji katika eneo hilo bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini kuwa ujenzi wa bwawa pekee utagharimu Shilingi 1,543,736,877.

Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini Mhe Edwin Mgate Dannda aliyetaka kufahamu ni lini andiko la mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Kijiji cha Mongoroma, Kata ya Serya wenye eneo la ekari 3000 utaanza utekelezaji wake, Mhe Mgumba alisema kuwa katika bajeti ya mwaka 2010/2011 Serikali kupitia Idara ya Umwagiliaji ilituma Shilingi milioni 300 kwa ajili kuendeleza miradi ya umwagiliaji ya Kisese, Kidoka na Mongoroma Serya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati huo.

Alisema Kati ya fedha hizo Shilingi 143,265,000 zilitumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu katika mradi wa Mongoroma Serya uliopo katika Kata ya Serya. Kazi zilizofanyika ni pamoja na upimaji wa sura ya ardhi (Topographical Survey), usanifu wa kina (detail design), matayarisho ya gharama za ujenzi, tathmini ya rasilimali maji (Hydrological survey), tathmini ya awali ya mazingira, utafiti wa udongo (Soil analysis) na masuala ya jamii.

Aliongeza kuwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Mongoroma Serya ulibaini kuwa bwawa hilo lingegharimu Shilingi bilioni 4 kwa wakati huo. Aidha, bwawa hilo lingekuwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekta 3,000 na kunufaisha zaidi ya wakulima 12,000 kwa ajiili ya kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya binadamu, unyweshaji wa mifugo na wanyama pori pamoja na ufugaji wa samaki katika vijiji vya Mongoroma, Serya na Munguri.

Mgumba alisema Serikali iko katika mchakato wa kufanya tathmini ya kina kwa miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kubaini thamani ya fedha, ubora wa miradi na mahitaji halisi ya uboreshwaji, uendelezwaji na kuchagua miradi michache kwa utekelezaji wa ujenzi kwa miradi yenye TIJA, matokeo na manufaa makubwa kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, baada ya tathmini hiyo na kutegemea upatikanaji wa fedha serikali itahakikisha bwawa hilo na skimu zingine zitajengwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...