Serikali ya Ufaransa kupitia Balozi yake nchini Tanzania imeahidi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na wadau wengine kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na malighafi zingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

Hayo yamesemwa na Balozi wa Ufaransa nchi Tanzania Mhe. Balozi Fredrick Clavier wakati wa ziara yake chuoni hapo iliyolenga kujifunza kuhusu Mradi wa Kilimo Hifadhi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa kwa kushirikiana na Shirika la Misaa la Switzerland (SWISSAID) na kutekelezwa na timu ya watafiti wa SUA, SAT na TOAM ambapo Ubalozi huo umechangia kiasi cha EURO 850,000. 

“Mradi huu ni wa miaka mitano unalenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo wapatao 6000 na kuhifadhi bayoanuai na mazingira kupitia uzalishaji kwa kutumia kilimo hai, matumizi sahihi ya mnyororo wa thamani wa kilimo hai, kuimarisha vikundi 269 vya wakulima wadogowadogo taasisi mwamvuli za vyama hivyo na kuweka kumbukumbu mbinu za kilimo hai zilizokubaliwa na wakulima ili kusaida utetezi wa kitaifa na kimataifa” Alisema Balozi Fredrick Clavier. 

Balozi huyo aliongeza kuwa katika mikakati yake anataka kuona kunakuwa na ushirikiano mkubwa kati ya wataalamu wa SUA na vyuo vingine kutoka nchini Ufaransa ambapo pamoja na mambo mengine wataalamu hao waweze kutembeleana wakiwashirikisha wanafunzi kwa lengo la kubadilishana uzoefu. 

Aidha, Balozi huyo amewataka wataalamu wa SUA, FAO, IRD na SWISSAID kukaa pamoja na kuangalia maeneo mawili au matatu ya mashirikiano katika utafiti na kuandika mradi wa pamoja na kisha kuuwasilisha kwake ili aweze kuuombea fedha kwenye Serikali yake maana hela ipo. 

Awali akitoa taarifa fupi ya kazi za SUA, Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda alisema kuwa Serikali ya Ufaransa ina historia ya muda mrefu ya SUA kwani imefadhili baadhi ya miradi hususani Mradi wa Kilimo Bustani na ujenzi wa jengo la kufundishia. 

“Ujio huu wa Balozi ni faraja kwa Chuo kwani ni hatua muhimu ya kufungua milango ya ushirikiano zaidi baina ya chuo na Serikali ya Ufaransa katika nyanja za utafiti na maendeleo katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inahimiza uwekezaji na kazi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025” Alisema Prof. Chibunda. 

Kwa upande wake Muwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bw. Fred Kafeero alisema kuwa FAO Tanzania wapo tayari kuingia kwenye ushirikiano huo na kwamba atatuma wataalamu kutoka ofisi yake ili waweze kukaa na timu ya watu watakaoteuliwa kuandaa mradi huo wa ushirikiano. 

Naye Mwakilishi Mkazi wa SWISSAID Tanzania bwana Blaise Burnier alisema wao wamesaidia wanafunzi wawili wa Shahada ya Uzamivu kwenye utafiti wao unaolenga masuala ya kilimo hifadhi ambao wanasoma SUA. 
Balozi wa Ufaransa nchi Tanzania Mhe. Balozi Fredrick Clavier (katikati) akiongea na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (kushoto).
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (kushoto) akizungumza na Muwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bw. Fred Kafeero (kulia) wakati wakimsubiri Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania.
Balozi wa Ufaransa nchi Tanzania Mhe. Balozi Fredrick Clavier (katikati), Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (kushoto), Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bw. Fred Kafeero (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...