Na Ripota Wetu, Michuzi TV

VIONGOZI wa Serikali kutoka Mkoa wa Ruvuma wameupongeza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill kwa uhifadhi misitu uliotukuka na ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa hatimae kutekeleza Tanzania ya Viwanda kwa utoaji malighafi endelevu ya mazao ya misitu kwa faida ya kizazi cha sasa na Vizazi vijavyo ikiwa ni pamoja na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.

Pongezi hizo zimetolewa mapema leo hii na ugeni uliotembelea shamba la miti Sao Hill ukiongozwa na Wakuu wa Wilaya za Songea, Namtumbo na Nyasa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Madiwani, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Kata, Vijiji na Wenyeviti wa vijiji sanjari na Wataalamu wa Misitu kutoka Shamba la Miti Mpepo waliotembelea shamba hili kwa lengo la kujifunza.

Akizungumza Ofsini kwake wakati wa mapokezi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi David William amesema kuwa shamba la miti Sao Hill limekuwa chachu kubwa ya uchumi wa wilayani Mufindi na Taifa kwa ujumla kwani limekuwa likikusanya mapato ya Serikali kupitia mazao ya misitu kwa kiasi kikubwa.

Ameongeza kuwa shamba hilo limekuwa likiendelea kuweka uhusiano mzuri na jamii inayozunguka shamba ili kuondokana na changamaoto zinazoweza kujitokeza kama vile moto wa msituni na migogoro ya ardhi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyansa Isabela Chilumba ambae pia ndie kiongozi wa Msafara huo akieleza malengo ya ziara amesema wameona ni vema kuja kujifunza katika Shamba la Miti Sao Hill kwani ni Shamba mama na ni shamba kubwa linalofanya vizuri hapa Tanzania.

Ameongeza kuwa ziara hiyo ni muhimu kwani wamejifunza kwa kuona namna ya shughuli za uvunaji zinavyofanyika, ufugaji wa nyuki na uchakataji wa asali, na kuona namna shamba linavyotoa ajira za muda mrefu na mfupi kwa jamii inayozunguka shamba sanjari na huduma za kijamii zinavyotolewa kwa jamii inayozunguka shamba.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema amesema Shamba hilo limekuwa la mfano wa kuigwa kwani limeweza kukusanya fedha zaidi ya Sh.bilioni 47 katika uvunaji wa miti kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na zaidi ya Sh.Milioni 700 kuanzia Julai 2018 hadi sasa katika zao la utomvu na hilo si jambo dogo.

Akisoma taarifa ya Shamba Kaimu Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill Bwana Daniel Silima alieleza kuwa shamba limeweza kukusanya zaidi ya Sh.bilioni 319 kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2008 hadi sasa na Tsh bilioni 6 kama CESS kuanzia mwaka 2010 hadi disemba 2018 kwa Halmashauri za Wilaya ya Mufindi, Mji wa Mafinga na Kilombero.

Aidha ameeleza Shamba limekuwa likichangia katika shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika jamii inayozunguka shamba kila mwaka kupitia utoaji wa miche ya miti bure kwa wananchi.

Ambapo kwa mwaka huu wa upandaji takribani miche ,Milioni 1 imegawiwa bure kwa wananchi wa mufindi na taasisi mbalimbali lakini pia , ujenzi wa barabara, madawati na kuchangia huduma nyingine za kijamii.

Katika ziara hiyo wageni kutoka Mkoa wa Ruvuma wamepata pia fursa ya kutembelea maeneo ya Shamba la Miti Sao Hill hususani katika maeneo ya ufugaji nyuki, eneo la uchakati wa asali, mnara wa mawasiliano kwaajili ya ulinzi wa msitu dhidi ya moto, bustani ya miche, na hatimaye kutembelea maeneo yanayovunwa utomvu kwa majaribio.

Shamba la Miti Sao Hill ndilo Shamba kubwa kuliko Mashamba yote 24 ya miti ya kupandwa ya serikali ambapo lina ukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwaajili ya upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira.

Shughuli za upandaji miti katika shamba hili zililianza kwa majaribio mnamo mwaka 1939 na kuonesha matokeo mazuri mwaka 1951 hivyo upandaji wa miti kwa kiwango kikubwa ulianza rasmi kuanzia mwaka 1960 hadi mapema miaka ya 1980.
 Wakuu wa Wilaya ya Namtumbo, Nyasa na Songea za mkoani Ruvuma walioambatana na wadau wa Shamba la Miti Mpepo lililopo mkoani humo kwenye ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Saohill wakipata maelezo kuhusu namna ambavyo miti inaandaliwa kabla ya kupandwa katika shamba hilo.
 Wakuu wa Wilaya ya Namtumbo, Nyasa na Songea za mkoani Ruvuma walioambatana na wadau wa Shamba la Miti Mpepo lililopo mkoani humo kwenye ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Saohill wakipata maelezo kuhusu shamba hilo.
 Sehemu ya miti ambayo imepandwa katika Shamba la Saohili
Msafara wa Wakuu wa Wilaya ya Nyasam Namtumbo na Songea mkoani Ruvuma wakielekea katika Shamba la Mitu Saohili ambako wamekwenda kuona namna ambavyo shamba hilo linavyosimamiwa kama sehemu ya kujifunza na kubadilisha uzoefu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...