Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka bayana msimamo na mwelekeo wake katika masuala ya Kilimo na Viwanda, Ulinzi na Usalama na Sayansi na Teknolojia katika muktadha wa mapambano ya kujikomboa kiuchumi na mwelekeo wa siasa za kidunia.

Akizungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ndg. Bashiru Ally Katibu Mkuu wa CCM amesema katika mazingira ya sasa ya kidunia mapambano ya kiuchumi yamejikita katika namna ambavyo nchi masikini zinasimamia ipasavyo sekta ya kilimo, uzalishaji wa kilimo wenye tija sambamba na viwanda vitakavyochakata bidhaa za kilimo na kujenga uwezo wa kuzalisha chakula, kujitosheleza ndani na ziada.

Ndg. Bashiru Ally amefafanua unyeti wa suala la ulinzi na usalama na kwamba vijana ndio walinzi wa mwanzo na wananchi kwa ujumla, hivyo uzalendo, nidhamu, kufanya kazi, utii na kujitoa ni misingi muhimu kwa vijana wa CCM. Aidha, ameeleza jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi hazitapokelewa vizuri na wasiotutakia mema na maadui zetu ambao wako ndani na nje ya nchi, na kwa mantiki hii vijana wa kitanzania wana jukumu ya kuilinda nchi yetu, kutetea msimamo wetu, kuyasemea mazuri yanayofanywa na Serikali yetu.

Akizungumzia kuhusu Sayansi na Teknolojia Ndg. Bashiru Ally Katibu Mkuu wa CCM ameeleza wigo wa Sayansi na Teknolojia ndio ulipo uwanja wa mapambano na ni muhimu kujihami mapema na kuwa tayari kukabiliana mashambulizi ya kimtandao, wanaotumia mitandao kupotosha kazi nzuri inayofanyika katika nchi yetu lazima wajibiwe kwa hoja na kwa ushahidi wakati wote.

Ndugu Bashiru Ally amewataka wajumbe wa Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la UVCCM kutupatia aina ya Kiongozi (Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka vijana) ambaye anaelewa mazingira tuliyomo na awe tayari kusimama imara kuulinda Muungano wetu, kujenga umoja, kulinda uhuru wetu, mtu mwenye msimamo usioyumba, atakayelinda heshima ya viongozi wetu na anayeakisi maono na mwelekeo wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vitendo vya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, vitendo vya rushwa, kila jambo linalokwenda kinyume na Katiba, Kanuni na desturi nzuri za Chama Cha Mapinduzi (CCM) havina nafasi katika Umoja wa Vijana wa CCM amesema Ndg. Bashiru Ally akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Maalum wa Baraza Kuu ya UVCCM.

Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la UVCCM unaketi kuchagua Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa anayewakilisha Umoja wa Vijana baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, umehudhuriwa na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi na Mzee Kombo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM pamoja na Viongozi wa UVCCM wakiongozwa na Ndg. Kheri James Mwenyekiti wa UVCCM.

Imetolewa na,

*IDARA YA ITIKADI NA UENEZI*
*CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)*

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...