Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Hali ya kiuchumi inayowakabili wagonjwa wengi wa maradhi
yasiyoambukiza Zanzibar imetajwa kuwa ni changamoto kubwa katika
kupata chakula sahihi cha kupunguza makali ya maradhi hayo.
Akitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na Kitengo cha maradhi
yasiyoambukiza katika mkutano wa wadau wa maradhi hayo, Mratibu wa
Kitengo hicho Omar Mwalimu alisema wagonjwa wa maradhi hayo wanatakiwa
kula zaidi matunda na mboga mboga na kupunguza kutumia mafuta na
vyakula vya uwanga.
Alisema katika utafiti huo wamegundua kuwa wananchi wengi wanaelewa
juu ya maradhi hayo na njia za kukabiliana nayo kupitia vyombo vya
habari na mikutano mbali mbali lakini hali ya kiuchumi ni kikwazo
kwao.
Alieleza kuwa tabia ya wananchi kuchelewa kufanya uchunguzi wa afya
zao mpaka wapate mabadiliko makubwa ya mwili ni moja ya tatizo
linalowakabili wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza nchini.
Omar Mwalimu alisema upatikanaji wa huduma za matibabu ya maradhi
yasiyoambukiza katika baadhi ya vituo vya shamba bado hairidhishi na
wagonjwa huvunjika moya na kwenda katika vituo hivyo na huamua kubaki
nyumbani ama kufuata huduma hizo Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa lipo kwa wagonjwa wenye tatizo la maradhi
ya Saratani kwa vile upatikanaji wa dawa za kutibu maradhi hayo ni
ghali na wagonjwa wengi hawana uwezo wa kuzinunua.
Hata hivyo Omar Mwalimu aliwashauri wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza
kutafuta ushauri wa madaktari waliosomea kabla ya kutumia dawa mbadala
ama kufuata tiba ya mitandao.
Alisema hivi sasa wamejitokeza wajanja wengi mitaani na kwenye
mitandao ya kijamii wanaotoa matibabu ya maradhi yasiyoambukiza lakini
hawana tiba sahihi ya maradhi hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Dk. Said
Gharib Bilal alisema maradhi hayo yapo na yamekuwa ni sehemu ya maisha
ya wananchi wengi, jambo la msingi ni kuwa na elimu ya kujua namna ya
kuishi nayo.
Baadhi ya waathirika wa maradhi yasiyoambukiza walioshiriki mkutano
huo uliofanyika Kitengo Shirikishi cha afya ya mama na mtoti
Kidongochekundu walisema mara nyingi wanapokwenda kutafuta dawa kwenye
vituo vya afya vya karibu vijiji, hawapati dawa ama hupata nusu ya
kiwango kinachohitajika.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (ZNCDA) Said Gharib Bilali akizungumza katika Mkutano wa wadau wa kujadili upatikanaji huduma bora za afya kwa wagonjwa wa maradhi hayo Zanzibar.
Mkuu wa Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Omar Mwalim akiwasilisha taarifa ya utafiti wa maradhi yasiyoambukiza katika Mkutano wa wadau uliofanyika Kitengo Shirikishi cha mama na mtoto Kidongochekundu.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa kujadili upatikanaji huduma bora za afya kwa wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza wakifuatilia taarifa ya utafiti uliofanywa kuhusu maradhi hayo.
Mshiriki Amour Kassim kutoka Jumuiya ya ZAMWASO akitoa
mchango katika mkutano huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...