Wazalishaji wa mazao ya nafaka nchini wahimizwa kuongeza thamani bidhaa wanazozalisha nchini na sio kuuza mazao ghafi ili soko liweze kuongezeka na kuleta faida katika sekta ya kilimo inayochangia katika ukuaji wa uchumi nchini. 

Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Richard Kasesela, Mkuu wa Wilaya wa Iringa alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa wazalishaji wa mazao ya nafaka nchini uliofanyika tarehe 3 Mei, 2019 mkoani Iringa uliondaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). 

Akiongea na washiriki zaidi ya 150 amesema sekta ya kilimo inaajiri watanzania zaidi ya asilimia 67 na kuchangia katika pato la Taifa kwa asilimia 30 na kuingiza dola bilioni 1.2 ambazo ni chache ukilinganisha na ardhi tuliyonayo na inalisha asilimia 65 ya malighafi katika sekta ya viwanda na zaidi ya asilimia100 katika chakula. 

“Kuna bidhaa hatujaziendeleza hadi sasa na zina fursa nzuri sana kwenye masoko nje ya nchi kama vile cornflakes na zinaliwa nchi nzima na hadi sasa Watanzania hawajaamua kuwekeza kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa hizi” alisema Mhe Kasesela 

Aliongeza kwa kusema kuwa msingi wa ustawi wa kilimo ni upatikanaji wa soko la uhakika, katika kutekeleza hilo serikali ya awamu ya tano imetengeneza mazingira rafiki kupitia uwekezaji wa viwanda kwa kutumia malighafi zake nchini 

Ameiomba TanTrade isaidie wafanyabiashara nchini katika kufundisha mikakati mbalimbali ya biashara hasa kwa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ili kuweza kufanya biashara kupitia simu za viganjani kupitia mifumo mbalimbali ya tehama. 

Alihitimisha kwa kutoa wito kuwa katika mkutano huo maazimio yajikite kwenye kutoa majibu ya ubora wa mbegu, namna ya uhifadhi bora wa mazao, kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua hasa katika maeneo yanayopitiwa na mito kwa kutumia maji machache, kuboresha mifumo mizuri ya kupata takwimu sahihi, masoko na pia kufanya mkutano huu uwe endelevu kila mwaka na katika kila maazimio yanayotolewa kwenye mkutano maafisa biashara, kilimo na ushirika wa serikali lazima washiriki ili kuweza kusaidia katika kusimamia na kutekeleza maazimio ya kila mkutano 

Bw Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade aliongeza kwa kusema kuwa mkutano huu utakuwa chachu kwa wazalishaji ili kuleta matokeo ya kuongeza uzalishaji, kuweza kutosheleza soko la ndani na kuangalia masoko katika nchi zinazotuzunguka katika ukanda wa Afrika Mashariki na nchi katika nchi wanachama wa jumuiya ya SADC 

Na amewasisitiza wazalishaji wa mazao ya nafaka nchini kushiriki katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambapo kutakuwa na mikutano ya wafanyabiashara (B2B) ili kuweza kupata masoko endelevu. 

Bw Ledis Kigala, Afisa Programu kutoka Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki aliongeza kwa kusema kuwa, Tanzania inauza mazao ya nafaka kama vile mchele, mahindi na maharage katika nchi jirani. Wakulima wameweka nguvu zaidi kwenye uzalishaji wa mahindi meupe wakati asilimia 90 ya mahindi yanayozalishwa duniani ni ya Njano. 

Pia alisema kuwa kuna fursa kubwa ya masoko kwa mazao ya nafaka hasa mahindi na mtama kwaajili ya matumizi ya viwanda vya bia ingawa hadi sasa changamoto kubwa katika sekta ya mazao haya ni uwepo wa sumu kuvu na uhifadhi bora wa mazao. 

Nae Bi Karungi Gotifrid, Afisa Ubora kutoka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko amewahimiza wakulima wa mazao ya nafaka kujiunga katika vikundi ili waweze kupewa elimu na alitoa vigezo vya mahindi yanayonunuliwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kama ifuatavyo unyevunyevu chini ya asilimia 13, mahindi yasiyokomaa chini asilimia 1, uchafu chini ya asilimia 1, mahindi yaliyooza na yenye ugonjwa hayatakiwi kuwepo ili kuepusha sumu kuvu, mahindi yaliyoliwa na wadudu hayatakiwi kuwepo kwasababu yanaondoa kiini ambacho kinahitajika kwa bianadamu vilevile mdudu hai haitajiki ndani ya magunia ya mahindi na pia mahindi yaliyovunjika yawe chini ya asilimia 1 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ni kweli serkar inatakiwa kutoa support kwa vjana ili waweze ongeza thaman ya mazao hasa nafaka

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...