KATIKA kushiriki shughuli za kimaendeleo Afisa tarafa wa Itiso ameitisha mkutano wa kimkakati uliolenga kuboresha shughuli za maendeleo katika kata zote za tarafa hiyo.

Akizungumza  katika kikao hicho Afisa tarafa wa Itiso Remidius Emmanuel amesema kuwa kufanyika kikao hicho kilichowakutanisha wataalamu wote kuanzia ngazi ya vijiji kimelenga kutoa mwelekeo mpya wa Tarafa hiyo  na kuwataka viongozi wote kuwa na sauti moja katika safari ya kuelekea Itiso mpya.

Afisa huyo amehimiza suala la uwajibikaji  na mshikamano kwa viongozi wote  kama msingi namba moja wa kuifikia "Itiso Mpya"

"Nafahamu kila mmoja wetu anafurahishwa na kazi kazi kubwa  inayofanywa  Rais wetu  Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, lakini naomba niwakumbushe jambo moja, tutahesabika tunamuunga mkono Mhe.Rais sio kwa maneno ya vinywa vyetu tu, bali ni kwa kutimiza wajibu wetu kupitia maeneo yetu,ikiwa tutafanya hivyo hapo tutakuwa tumemuunga mkono Mhe. Rais."  Ameeleza.

Pia amesema kuwa Kilimo na Ufugaji vipewe kipaumbele katika tarafa hiyo.
 "Shughuli kubwa ya uchumi wa tarafa yetu ni kilimo na ufugaji ndio maana nimehitaji uwepo wa Maafisa Ugani na Maafisa mifugo wa tarafa ya Itiso katika kikao hiki, nataka muone dhamira yangu,tunahitaji kubadili uchumi wa tarafa hii kupitia sekta hizo na hii itasaidia kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kuchochea sekta nyingine, tutaelekeza nguvu na mikakati katika eneo hili, na kwa kweli nimedhamiria" ameeleza.

Amesema maendeleo ya Itiso yanategemea Ushirikiano wa pamoja na amewataka viongozi wote kuwa waadilifu, kusimama na kufuatilia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuhakikisha viongozi wote wanawafikia wananchi na kutatua migogoro na kero za wananchi pamoja na kuendelea kutekeleza mipango na maelekezo ya Serikali kwa ngazi zote.

Kuhusu kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Afisa tarafa huyo ameeleza kuchukizwa na baadhi ya Serikali za vijiji ambazo zimeendelea kutoitisha mikutano mikuu ya vijiji na  kushindwa kusoma mapato na matumizi kwa visingizio kadhaa na kuagiza ifikapo Julai 30 mwaka huu vijiji vyote viwe vimeitisha mikutano hiyo na kusoma mapato na matumizi  na kuahidi kufuatilia hatua hiyo.

"Nina taarifa baadhi ya vijiji kutoitisha mikutano mikuu ya vijiji na mnakwepa kusoma mapato na matumizi, kila mara mnajizungusha na kusingizia kwamba watu hawaji mikutanoni, jambo hili nitalisimamia" amesisitiza.

Hata hivyo amehimiza viongozi wote kuendelea kutumia elimu, maarifa na uzoefu wao kuleta tija katika maeneo yao na kuwa wabunifu, aidha  amefungua milango ya kupokea ushauri,maoni na mapendekezo ambayo yatalenga kuiletea maendeleo tarafa ya Itiso.

Baadhi ya Viongozi waliopata nafasi ya kutoa maoni yao wamefurahishwa na mipango hiyo huku wakimpongeza kiongozi huyo na kuahidi ushirikiano mkubwa na baadhi yao wakionekana kufurahishwa zaidi na hatua ya  kurejeshwa kwa mashindano ya sanaa za  utamaduni na mpango wa  kuinua vipaji mbalimbali kupitia michezo na burudani Sambamba na utoaji wa Motisha kwa watumishi wote wanaofanya vizuri katika utendaji wao wa kazi na kuweka  utaratibu wa  kuwapa zawadi Wanafunzi wote katika shule za msingi na sekondari wanaofanya vizuri kitaaluma.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Polisi Tarafa ya Itiso Inspekta Misana Makweba pamoja na mambo mengine amewataka viongozi hao kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na kueleza  kwamba Ulinzi na Usalama wa Tarafa ya Itiso uko mikononi mwa wana Itiso wenyewe na kuongeza kuwa wapo baadhi ya Viongozi wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa za kuwafichua wahalifu  kwa  matukio kadhaa.

 Diwani wa Kata ya Dabalo Elisha  Matewa  amesema  tarafa ya Itiso kupitia kata ya Dabalo ina matukio makubwa ya  kihistoria ambayo yameanza kusahaulika, hivyo mkakati wa kuanzisha utaratibu wa kuhifadhi historia na kumbukumbu za Tarafa ya Itiso ni jambo jema sana na kupongeza sana suala la kutambua na kuenzi utamaduni wetu hatua itakayo anza kurejesha maadili yanayoporomoka kwa kasi.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya viongozi wote waliohudhuria  kikao hicho Diwani wa kata ya Haneti Peter Chidawali  amempongeza  Afisa Tarafa huyo kwa kutoa taswira mpya kwa tarafa hiyo  na wao kama Madiwani wanahaidi     ushirikano kwa kiongozi huyo.

Tarafa ya Itiso ni miongoni mwa Tarafa Tano (5) za Wilaya ya Chamwino zinazipatikana katika mkoa wa Dodoma.
 Afisa Tarafa Itiso Bw. Remidius Emmanuel akizungumza na viongozi mbalimbali wa Tarafa hiyo kupitia  kikao maalum kilichohitishwa na kiongozi huy uliolenga kuboresha shughuli za maendeleo katika Tarafa ya Itiso.
 Diwani wa Viti maalum Tarafa ya Itiso  Mhe. Hajira Mdimu akizungumza kupitia kikao hicho.
Baadhi ya Viongozi waliohudhuria kikao hicho

Mkutano ukiendelea

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...