Muendelezo wa Kazi za ujenzi wa Mtaro Mkuu wa kupitishia Maji ya Mvua
kuunganisha kipande kilichobakia cha Mita kati ya Mia 700 hadi Mia 750
kilichopo baina ya Mikunguni na Sebleni unatarajiwa kuendelea tena
kuanzia Tarehe 20 mwezi huu.
Kazi hiyo inayotazamiwa kufanywa ndani ya kipindi cha Miezi Mitatu
ilisita kwa muda kutokana na utepetepe wa ardhi uliosababishwa na Mvua
kubwa za Masika zilizopita na kupelekea kifaa cha kuchimbia kupata
changamoto ya kufanyakazi ipasavyo.
Akitoa ufafanuzi wa Ujenzi wa Mtaro huo mbele ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Mikunguni, Meneja wa Mradi
wa Huduma za Jamii Mijini { ZUSP} Nd. Makame Ali alisema tatizo la
kutuama kwa Maji ya Mvua katika meneo ya Mji wa Zanzibar linatarajiwa
kuondoka baada ya kukamilika kwa Mradi huo.
Balozi Seif alifanya ziara hiyo maalum kuangalia athari zinazotokana
na Ujenzi wa Miundombinu hiyo ya Mtaro kufuatia malalamiko kadhaa
aliyokuwa yakitolewa na Wananchi hasa mawasiliano ya bara bara yasiyo
rafiki kwa wasafiri wa vyombo tofauti vya moto katika kipindi hichi.
Nd. Makame alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
kuunganishwa kwa kipande hicho cha Mita Mia 700 kutaonyesha
matumaini ya kumalizika kwa Mtaro huo unaotokea Bwawa la
Mwanakwerekwe, kupita Bwawa la kwa Mtumwa Jeni, kuelekea Bwawa la
Sebleni kupitia Mikunguni na hatimae maji ya Mtaro huo kumalizia
Bahari ya Kinazini.
Alisema kutokana na uchimbaji wa Mtaro huo kwenda chini umbali mkubwa
zaidi ya Mita Nane Wahandisi wa Ujenzi wako wanalazimika kuwa makini
katika kuchukuwa tahadhari ya Usalama wa Watu ambao ni jambo la
msingi.
Akizungumzia Bara bara za Lami zilizopitishwa Mtaro huo Nd. Makame
alisema Wahandisi wa Mradi huo kwa mujibu wa Mkataba wana jukumu la
kujenga upya bara bara hizo ili kurejesha uhalisia uliokuwepo wa
Miundombinu hiyo ya Mawasiliano.
Alisema changamoto inayokwaza kazi hiyo kwa hatua ya Awamu ya kwanza
ya ujenzi wa Bara bara kwenye maeneo yaliyopita Mtaro yaliyokamilika
ni uhaba wa kifusi cha kuweka sawa maeneo yaliyoathirika.
Alieleza kwamba juhudi za kuomba kifusi katika Taasisi zinazohusika
zimeshachukuliwa na hadi sasa kilichopatikana kimefikia Cubic Mita Mia
150 wakati mahitaji halisi ya kufanikisha kazi hizo kipatikane Kifusi
chenye ujazo wa Cubic Mita Elfu 14,000.
Kuhusu mtaro wa zamani wa maji ya mvua uliokuwa ukitumika kutoa maji
katika Bwawa la Sebleni Meneja wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini {
ZUSP} Nd. Makame Ali alisema jitihada zitafanywa katika kuufanyia
marekebisho madogo Mtaro huo ili uendelee kutoa huduma kama kawaida.
Nd. Makame alisema marekebisho hayo yatawezesha maji yote ya Mvua
yanayotiririka kutoka maeneo mbali mbali ya Mitaa ya Ng’ambo
yaliyojirani na Mtaro huo maji yake yatiririke na kuingia Mtaro Mkuu
katika eneo la Kwa Abass Hussein.
Akiridhika na kazi kubwa ya mafanikio iliyofanywa na Wahandisi wa
Ujenzi wa Mtaro huo Mkuu wa Maji ya Mvua, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ni vyema kwa Wataalamu wa Ujenzi
kuwa na utaratibu wa kuwaeleza Wananchi hatua wanayofikia katika
Miradi wayayoitekeleza.
Balozi Seif alisema utaratibu huo utasaidia kuondosha malalamiko
yanayotolewa na Wananchi hasa pale wakati wa ujenzi wa Miundombinu
unaposita na kuleta usumbufu kwao bila ya kupatiwa Taarifa yoyote.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Maeneo yaliyopita Mtaro huo
Mkuu wa Maji ya Mvua, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed
Mahmoud alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kuwaelimisha Wananchi
kujenga Utamaduni wa kufuata utaratibu wa hifadhi ya Taka taka
Mitaani.
Mh. Ayoub alisema kuachiliwa kuzagaa ovyo kwa taka taka mbali ya
kutishia afya za Wakaazi wake lakini pia kunaweza kusababisha
uharibifu wa Miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa gharama kubwa ili
iwahudumie Wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika ziara hiyo alipata wasaa wa
kuangalia eneo la Mtaro hapo Mikunguni ambalo haliko rafiki kwa
Waendesha vyombo vya moto kipindi hichi, kuangalia Mtaro hapo Kwa
Abass Hussein na kutumia muda wa kuukagua hadi ulikoishia katika eneo
la Kinazini.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkuu wa Moa
Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud wakikagua Mtaro Mkuu wa Maji
ya Mvua katika eneo la Kwa Abass Hussein hadi Kinazini.
Muonekano
wa Barabara ya Mikunguni iliyofumuliwa kwa kupitisha Ujenzi wa Mtaro
Mkuu wa Maji ya Mvua unaoelekea Kwa Abass Hussein na kuishia Kinazini.
Mhandisi
Mshauri wa Ujenzi wa Madaraja Mhandisi John Nyaroko akimfahamisha
Balozi Seif hatua zinakazochukuliwa za kutia zege kwenye Daraja la
Kinazini kunusuri kasi ya Maji ya Mavua yatakayokuwa yakipita kwenye
Mtaro Mkuu. Picha na – OMPR – ZNZ.
Balozi
Seif akiwaagiza Waandisi wa Miradi ya Ujenzi Nchini kutoa Taarifa kwa
Wananchi hatua za utekelezaji wa Miradi yao kila wakati hasa pale
inapotokezea hitilafu ya kukwama kwa Miradi hiyo.
Meneja
wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini { ZUSP} Nd. Makame Ali akimueleza
Balozi Seif hatua zitakazochukuliwa kumaliza Mtaro Mkuu wa Maji ya Mvua
hapo Mikunguni kipande kidogo kilichobakia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...