Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji mkubwa wa kuondoa vivimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo (cerebral aneurysms) kwa mgonjwa aliyekywa akisumbuliwa na tatizo hilo.
Kufanyika kwa upasuaji huu ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi na kuhakikisha matibabu ya ubingwa wa juu yanatolewa hapa nchini.
Upasuaji huu umechukua muda wa takribani saa sita na umefanywa na wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari Bngwa Mshauri wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Prof. Huh Seong kutoka Yonsei, Korea Kusini.
Kwa mujibu wa Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Dkt. Raymond Makundi, Hospiali ya Mloganzila inakua ya pili kwa hospitali za umma hapa nchini kufanya upasuaji huu wa kibobezi.
“Awali wagonjwa waliohitaji huduma hii walikuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na uchache wa wataalam na ukosefu wa vifaa tiba, hivyo kwa mgonjwa kama huyu mmoja ambaye tumemfanyia upasuaji endapo angepelekwa nje ya nchi ingegharimu zaidi ya shilingi milioni 40 ikiwa ni gharama za upasuaji, usafiri, malazi pamoja na msindikizaji,’’ amesema Dkt. Makundi.
Tatizo la vivimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kurithi vinasaba ambavyo mtu huzaliwa navyo, uvutaji wa sigara na maambukizi ya vijidudu kama bakteria vinavyoathiri mishipa ya damu.
 Ugonjwa huu huchelewa kugundulika kutokana na watu kutokufahamu dalili zake, upungufu wa vifaa vya uchunguzi pamoja na watalaam kuchelewa kubaini tatizo hilo mapema. Baadhi ya dalili ni kupata maumivu makali ya kichwa, kuona vitu viwili viwili (double vision) na kupoteza fahamu.
Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Dkt. Alvin Miranda amesema lengo la upasuaji ni kufunga vivimbe hivyo kwa kutumia vifaa tiba maalum (aneurysm clips) ili kuzuia damu isiendelee kuvuja katika ubongo.
“Mgonjwa anapopata tatizo la kuvuja damu kwenye ubongo kwa mara ya kwanza anakua katika hatari ya kupoteza maisha kwa asilimia 30 na endapo akivuja damu kwa mara ya pili hali hii inaweza kusababisha kifo kwa asilimia 70 hadi 80,” amefafanua Dkt. Miranda.
Takwimu zinaonesha wastani wa asilimia 3 ya watu duniani hupata tatizo hilo kila mwaka na nusu kati yao, wanawahi kufika hospitalini baada ya mishipa kupasuka, huku wenginge wakipoteza maisha kabla ya kufikia huduma.
Kwa upande wake, Prof Huh Seong amesema Hospitali ya Yonsei ya Korea Kusini itaendelea kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kubadilishana utaalam na kupanua huduma hizi za kibobezi katika magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu ili kuzifanya ziwe endelevu katika hospitali za umma.
 Madaktari bingwa wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Alvin Miranda (wa kwanza kulia) na Dkt. Raymond Makundi (wa pili kulia) wakiwa katika hatua ya kwanza ya upasuaji.
 Daktari Bingwa Mshauri wa Upasauji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Korea Kusini, Prof. Huh Seong (katikati) akishirikiana na wataalam wa Hospitali ya Mloganzila katika upasuaji wa ubongo wa kuondoa vivimbe vilivyopo kwenye mishipa ya damu ndani ya ubongo (surgical aneurysm clipping).
 Daktari Bingwa mshauri wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kutoka Korea Kusini, Prof. Huh Seong (aliyevaa miwani) akifafanua jambo kuhusu upasuaji wa kuondoa vivimbe kwenye ubongo. Kushoto ni Bi. Cosila Tambila ambaye amefanyiwa upasuaji huo na wa kwanza kulia ni Dkt. Alvin Miranda akifuatiwa na Dk. Raymond Mkaundi.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (kulia) akielezea mipango ya hospitali katika kuendelea kutoa huduma za kibingwa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa huduma Dkt. Mohamed Mohamed.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...