Na,Moshy KiyungiTabora.

Michael Enoch, alivuma sana hususan alipokuwa akipiga muziki katika bendi za Juwata, Western Jazz na Mlimani Park Orchestra za jijini Dar es Salaam.

Miaka ya 1980 na 1990, jina la ‘Ticha’ lilikuwa likitajwa sana kwenye kumbi za sterehe ambako bendi za Juwata na DDC Mlimani Park Orchestra zilikuwa zikitoa burudani maridadi.

Ilikuwa mara baada ya kutamkwa, katikati ya wimbo husika, sauti ya Muhidin Gurumo inasikika ikiita “Aah King Michael”.

King kwa lugha ya Kiswahili ina maana ya Mfalme. Michael aliitwa King lakini hakuwa na dola, ila uwezo wake katika muziki, ‘akabatizwa’ wadhifa huo. Ikumbukwe kwamba Mhidin Maalim Gurumo, alipiga muziki katika bendi zote hizo mbili.

Vijana wa miaka ya karibuni hawakuwahi kumshuhudia Michael Enoch akiwa jukwaani, kupitia makala hii watasoma na kuweza kuona juhudi za wanamuziki walioipaisha tasnia ya muziki wa dansi wakati huo.Enzi zake alikuwa akiuweka ‘muwa’ mdomoni kupuliza, ukumbi ulikuwa ukizizima kwa shangwe, kwa jinsi alivyokuwa akiwakosha.

King Michael alilinganishwa na Manu Dibango kwa upulizaji wa Saxophoni.
Sifa za kuitwa Ticha, si kama alikuwa akiingia darasani kufundisha, bali alikuwa na Weledi wa kupiga kila ala ya muziki. Pia manju wa kutunga na kuimba nyimbo wakati mwingine.

Hata hivyo kuitwa Ticha (mwalimu), iliwezekana kabisa, alikuwa mwalimu wa ukweli kutokana na kuusomea muziki tangu akiwa shule ya msingi.Akielezea juu ya Wasifu wake, King Michael alisema yeye anatoka katika kabila la Wawemba, lililopo nchini Zambia.

Alizaliwa Oktoba 1942, katika kijiji cha Luansha, nchini humo na kupewa jina la Michael Enoch Chinkumba.Historia yake katika muziki alieleza kuwa alianza kupiga muziki mwaka 1958, akiwa nchini Zambia.

Ticha Michael aliwahi kueleza kuwa pamoja na kuutumikia muziki kwa kipindi kirefu, hakuweza kujivunia matunda ya kazi yake.

Cha muhimu kwake ni kujivunia kuona wanamuziki wengi walipitia mikononi mwake hususan katika kipindi cha miaka ya 1960.

King Michael alisema kipindi hicho kulikuwa na upinzani kati ya bendi za Dar es Salaam Jazz na Western Jazz uliokuwa umechukuwa nafasi kubwa.

Western Jazz kulikuwapo na miamba katika muziki, mmojawapo alikuwa mwanamuziki Wema Abdallah, alieleza kuwa alikuwa mcharaza gitaa mahiri.

Ticha Michael aliwahi kueleza kuwa pamoja na kuutumikia muziki kwa kipindi kirefu, hakuweza kujivunia kula matunda ya kazi yake.

Cha muhimu kwake alijivunia kuona wanamuziki wengi walipitia mikononi mwake hususan katika kipindi cha miaka ya 1960.

Baadaye Michael Enoch alikwenda kujiunga katika bendi ya Dar es Salaam Jazz iliyokuwa ikipiga muziki wake kwa mtindo wa ‘Mundo’ na walijulikana kama ‘Majini wa Bahari’.

Aliweza kuingoza vyema bendi hiyo, ikawa tisihio katika jiji la Dar es Salaam wakati huo.

Baada ya kuitumikia kwa kipindi kirefu, aliondoka akaenda kujiunga katika bendi ya Dar es Salaam International, iliyokuwa ikiongozwa na Marijani Rajabu.

Alikuwa Abel Balthazar aliyemchomoa Ticha Michael Enock kwenda kuwa miongoni mwa wanamuziki walioasisi bendi ya Mlimani Park Orchestra mwaka 1978.

Wengine alioambata nao ni pamoja na pamoja na Joseph Bernard, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’, Abdalah Gama, Kosmas, Chidumule, Machaku Salum na Habib Jeff.

King Encoh aliuzungumzia muziki wa zamani na wa sasa, akisema tungo za sasa zinalipuliwa, hazipangiliwi na hata midundo inakolezwa na madoido mengi ya nje.

Alisema kuwa utaratibu huo unaweza ukapelekea kuwa mwisho mbaya kwa nyimbo, bendi na hata watunzi wenyewe.

King Michael alisema ingawa yeye alisomea muziki tangu miaka ya 1950, lakini wakati walipotaka kwenda kurekodi Redia Tanzania Dar es Salaam (RTD) wakati huo, Mashairi yao yalipitiwa upya na wakati mwingine kurejeshwa kwenye bendi kwa ajili ya marekebisho.

Hali hiyo ilionekana kana kwamba ilikuwa ni ukiritimba, lakini iliboresha tungo nyingi za wanamuziki.

King Michael alijaaliwa kipaji cha muziki tangu akiwa mtoto mdogo, Nyakati za mapumziko kijijini kwao Luansha, alikuwa akijishughulisha kutengeneza gitaa la makopo aliyoyafunga nyuzi nyembamba kisha kuanza kupiga.

Kaka yake aliyemtaja kwa jina la Steven kwa bahati nzuri alikuwa amenunua gitaa la Galatone.

Pia alikuwa na rafiki yake Boston Masatunya, ambaye naye kaka yake alimnunulia gitaa aina ya Gibson, ambalo lilikuwa la besi.

Mapenzi yao katika muziki wakiwa katika shule ya msingi ya Luansha walikomaliza mwaka 1958, wakaanza kupiga muziki wa maonesho nyakati za usiku hasa mwisho wa wiki.

Kikundi chao kilijulikana kama Music Brothers Concert Group, kilichowajumuisha akina dada watatu Adesi, Rhoda na Pani. Rafiki yao mwingine Godwin alikuwa akipiga drums.

King Michael aliendelea na kikundi hicho, lakini mwaka uliofuata akina dada hao wakaanza kupata wachumba wakaoelewa.

Michael Enoch akiwa kiongozi, akaamua kuachia ngazi, akaenda kujiunga katika bendi kubwa iliyojulikana kama Luansha Band.

Ticha aliwahi kueleza kuwa pamoja na kuutumikia muziki kwa kipindi kirefu, hakuweza kujivunia kula matunda ya kazi yake, bali aliridhika kuona wanamuziki wengi walipitia mikononi mwake hususan katika kipindi cha miaka ya 1960.

Mnamo mwaka 1960 aliyekuwa mdhamini wa Chama cha Tanganyika Nation Union (TANU), marehemu John Mwakangale, alifika nchini kwao Zambia.

Mwakangale akiwa nchini humo, aliona uwezo wa Michael Enoch wakati huo alikuwa kijana sana.

Michae Enoch akawashawishi wadogo zake Godfrey na Elias, aliyekuwa DC wa Mbeya, wanunue vyombo, waende mjini Mbeya.

Wakaunda bendi yao iliyokuwa ikiitwa Three Brothers Band, wakiwa na lengo kubwa la kuleta ushindani dhidi ya bendi ya Mbeya Jazz.

Bendi yao ilikuwa imesheheni wanamuziki wageni tupu. Wazambia walikuwa yeye Michael Enoch, Boston Masantunya, Saizi na Godwin.

Wamalawi walikuwa akina John na Felix wakati Wazimbabwe walikuwa akina John Tagoma, Mwasibanda na Thomas.

Lakini mwaka huohuo baada ya kufanya maonyesho katika miji ya Mbeya, Chunya, Tabora na Mwanza, bendi hiyo ikafa, tena kifo kibaya sana.

Michael Enoch alibainisha kuwa wakati wakiwa katika mji wa Mwanza wakati huo, waliibiwa vyombo vyote vya muziki.

"Tuliibiwa vyombo vyote vya muziki mjini Mwanza wakati tukijiandaa kwenda kupiga mjini Musoma… tulipakia vyombo kwenye Canter moja, dereva akasema kwamba, nisubirini nikajaze dizeli kwenye gari, lakini kumbe alikuwa mwizi, akatokomea na vyombo…” alisema Ticha Michael Enoch akionesha masikitiko makubwa.

Lakini kama Wahenga walivyonena kuwa “Mwenye bahati habahatishi” usemi huo alijionesha wazi kwa King Enoch ambaye alipata bahati nyingine ya kuazimwa vyombo vya muziki na bendi ya Cuban, iliyokuwa na makao yake makuu katika mji wa Tabora. Bendi hiyo ni tofauti na ile Cuban Marimba ya Morogoro.

Kuingia Dar Jazz.

Baada ya kupata vyombo hivyo walichukuliwa mahsusi kwa ajili ya maonesho kadhaa huko Nzega.

Wakati huohuo mwanamuziki wa Dar es Salaam Jazz, Bi. Balimi Ally, alifika Nzega akiwa njiani kwenda Ukerewe, Mwanza kumfuata mpiga solo wao Ausi.

Akaelezwa kuwa hapo Nzega kuna mwanamuziki mzuri sana anapiga muziki, akaamua kwenda kumshuhudia.

Baada ya kumuona Michael Enoch akipiga solo vizuri, Bi. Balimi akafanya mazungumzo ya kumrubuni King Enoch ili akakubali kuondoka naye.

Michale Enoch alikubali ghiriba za mama huyo, usiku huohuo wakapanda treni kwenda Dar es Salaam pamoja na Mzambia mwenzake aliyekuwa na jina la Saizi aliyekuwa akipuliza saxophoni.

Walipofika Dar es Salaam, wakakabidhiwa kwa uongozi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz, iliyokuwa ikimilikiwa na Mzee Muba.

Bi. Balimi alikuwa akiaminika katika bendi ya Dar es Salaam Jazz kwa uwezo waka wa kumshawishi mwanamuziki yeyote, akakubali kujiunga na bendi yao.

Aliwahi kumsimulia mwandishi wa makala hii jinsi alivyofaulu kumpata Michael Enoch na kumfikisha katika uongozi wa bendi ya Dar. Jazz.

Bi. Balimi Alli akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, alisema kuwa ilikuwa kama sinema jinsi alivyoweza kumnasa King Michael Enoch mjini Nzega.

Wakati akielezea historia hiyo, miaka ya 1990, bendi ya Dar es Salaam Jazz ilikuwa amekwisha kufa, yeye alikuwa ameachana na mambo ya muziki, akawa akitumia muda mwingi kuswali, huku akijutia yote aliyokuwa akiyafanya kipindi cha nyuma.

Katika bendi Dar es Salaam Jazz kulikuwepo na wanamuziki akina Hamisi Nguru, Bi. Bilimi Ally, Ally 'Chongo', Shaban Mangano na yeye King Enoch waliokuwa wakicharaza gitaa la solo.

Walikuwapo wanamuziki wengine akiwemo mpiga tumba Nasoro, Edward Salvi na Gray Sindo waliokuwa wakipuliza saxophone.

Bendi hiyo baadaye iliongeza nguvu kwa kumchukuwa Juma Akida, aliyekuwa mtunzi na mwimbaji.

Mwaka 1968 ulishuhudia kujiunga kwa wanamuziki wengine wakiwemo waimbaji Issa Ntini na Omar Seya, Makwaya Sudi aliyekuwa akipiga besi, Meckline Ibrahim kwa upande wa rhythm, Ramadhan alikuwa kwenye solo namba, Kulwa Thomas alikuwa akizicharanga drum na Zimataa aliyekuwa akizidumda tumba.

Kulikuwa na wapuliza midomo ya bata (saxophoni) Majengo Selemani, Albino na Abdallah Kimeza.

Wana Mundo wakati huo walikuwa wakitamba na nyimbo za Dada twende tukalime’ Mbuzi, Kama kisu utajichoma mwenyewe, Dada karibu kwetu, Heko Mwalimu Nyerere, Haifai kusimama juu ya milima, Haya yote ni ya dunia, Nitawaachia wenzangu na Mary Kamata.

Nyimbo hizo zote zilitungwa na King Michael Enoch.

Juma Akida naye aliibuka na nyimbo za Mtoto acha kupiga mayowe na Michael hapendi Ugomvi, ambazo zilirekodiwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD).

Mwaka 1972 wakaenda nchini Kenya katika studio za Chandarana kurekodi nyimbo za Kama Kisu utajichoma mwenyewe, Mbuzi, Lydia umenitoroka na Mary Kamata.

Kwa majaaliwa ya mungu mwaka huohuo bendi yao ilipatwa na pigo jingine baada ya mmiliki wake Mzee Muba kufariki dunia.

Hussein Kawambwa akapewa nafasi ya kuiongoza bendi hiyo.

Ili kuongeza nguvu, uongozi uliwachukuwa wanamuziki wengine wakiwemo wapiga magitaa ndugu wawili Saulo Ndumbaro aliyekuwa akipiga gitaa la besi na Duncan Ndumbaro, kwenye gitaa la rhythm.

Wanamuziki wengine walikuwa Hamisi Abdallah aliyekuwa mwimbaji, Mathias alikuwa akipuliza saxophone, Komsoni na Abeid na Ramadhan Shomvi walikuwa wakipiga tumba.

Bendi ya Dar es Salaam Jazz ikaanza kutumia mtindo wa Pachanga.

Uchakavu wa vyombo mwaka 1978 mambo kuwa si mazuri kwao, lakini mwaka huohuo kukaanzishwa bendi ya Dar International iliyokuwa ikimilikiwa na Zakaria Ndabamei, aliyekuwa akiishi Tanga.

Bendi hiyo ikatumia mtindo wa Super Slow.

Miongoni mwa wanamuziki waanzilishi walikuwa Marijani Rajabu Marijani, Cosmas Thobias Chidumule, Ally Rajabu, Salehe ‘Belesa’ Kakere, Mzambia mwenzake Joseph Mulenga ‘String Master’ kwene gitaa la besi, Abel Balthazar kutoka katika bendi ya Nuta Jazz aliyekuwa akipiga gitaa la solo, Michael Enoch kwenye sax, Abdallah Gama alisimama kwenye gitaa la rhythm na Haruna Lwari alikuwa kwenye tumba.

Wengine walikuwa akina Saidi kwenye drum, Joseph Bernard akipuliza sax, Machaku Salum, Ibrahim Mwinchande na Betto Julius waliokuwa wakipuliza tarumbepeta,.

Bendi hiyo ikaibuka na vibao vitano, Rufaa ya Kifo kilichotungwa na Kosmas Chidumule na kuimbwa na Marijani Rajabu, Nyerere Baba Mlezi na Mwana rudi wee ambazo ni utunzi wake Joseph Mulenga, Margreth msikilize shangazi Belesa Kakere, Sikitiko aliotungwa na Marijani Rajabu.

Licha ya kuwa na ‘vifaa’ vyote hivyo, bendi ilidumu kwa takriban miezi miwili tu kisha ikafa.

Kifo cha bendi hiyo kilitokea baada mmiliki wake kutoelewana na Wanamuziki wote isipokuwa Marijani Rajabu.

Wanamuziki hao wakaondoka kuanzisha bendi ya Mlimani Park Orchestra, iliyokuwa inamilikiwa na Tanzania Transport & Taxes Services - TTTS.

Wanamuziki wengine waliokuja kuanzisha hiyo ya Mlimani Park ni Muhidin Maalim Gurumo, Hassan Rehani Bitchuka, Juma Hassan 'Town', Suleimani Mwanyiro na Abdallah Omar 'Dullah' wote kutoka bendi ya Msondo Ngoma.

Mlimani Park Orchestra ikaibuka na nyimbo tatu za kwanza ambazo zilikuwa Celina, uliotungwa na Joseph Mulenga, Barua kutoka kwa mama utunzi wak Kosmas Chidumule na Kassim Kafilisika, uliotungwa na Mhidin Maalim Gurumo.

King Enoch alidumu na bendi hiyo kwa miaka yote mpaka mauti yalipomfika mwaka 2004.

Baadaye King Michael akaanza kuzongwa na maradhi, akawa anashindwa kupanda jukwaani kuimba katika siku za mwishoni mwa maisha yake.

Kwa uungwana wake Michael Enoch Chinkumba aliwashukuru Watanzania kwa kusema “Watanzania wote ni ndugu zangu, kwa kuwa wamenilea. Niliondoka kwetu Zambia miaka 42 iliyopita, sijaenda tena mpaka leo. Wazazi wangu walikufa wakati nikiwa shule ya msingi na ndugu zangu kila mmoja yuko kivyake..Nawashukuru nyote aidha ninaishukuru sana Sikinde kwa kunithamini mpaka leo hii…”

Katika siku za mwisho, alikuwa akihudhuria mazoezi kwa kazi ya kupangilia muziki.

Bendi hiyo Mliamani Park Orchestra ilikuwa inamthamini na kumpatia matibabu na mshahara wake King Michael kama kawaida.

Kwa sababu ambazo hazikuelezwa zinaeleza kuwa King Enoch hakubahatika kuoa mke, lakini alipata kuzaa watoto wawili, mmoja bahati mbaya alifariki, wa pili Iddi Enoch.

King Michael ni mfano wa kuingwa kwa wanamuziki wengine kujifunza uvumilivu pia kugawa weledi walionao kwa wengine.
WANAMUZIKI  WA BENDI YA DAR JAZZ WAKITOA BURUDANI.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...