Mwaka jana wakati wa Bunge la bajeti serikali ilipiga hatua kubwa yenye mwelekeo sahihi wa kupunguza gharama anazoingia msichana na mwanamke kwenye kununua bidhaa za kujihifadhi wakati wa hedhi. Serikali ilitoa msamaha wa kodi (VAT 18%) kwa bidhaa za pedi, uamuzi ambao wengi tuliufurahia. 

Lakini mwaka mmoja baada ya kutolewa kwa kodi, serikali imeirudisha tena kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutokana na kudai kuwa wafanyabiashara hawajapunguza bei kama ilivyokusudiwa.

Maoni yangu

Katika sera yoyote ambayo serikali inapitisha ni lazima serikali iwe mbele kwenye kuweka mikakati ya ufuatiliaji ili sera husika iweze kuzaa matunda na kuwanufaisha walengwa. Tumeona kwa mfano hata serikali ilipotaka kila mfanyabiashara awe na EFD mashine, wote hawakukubali kutekeleza kwa wakati mmoja. 

Lakini serikali ilikuwa na mikakati ikiwemo elimu kwa wafanyabiashara ya kwa nini ni muhimu kuwa na EFD mashine, na leo tunaona wafanyabiashara wengi wana EFD mashine, ingawa pia inawezekana wakawa sio wote. Je, serikali ilirudisha utaratibu wa wafanyabiashara kutokuwa na mashine kwa sababu tu ndani ya muda mfupi hawakutii sheria na kuinufaisha nchi na mapato? Hapana. 

Haya tumeona hata kwenye masuala mengine ambayo serikali imeyaanzisha kwa lengo la kunufaisha nchi kwa mapato na kusaidia walaji kama vitambulisho vya wafanyabiashara (na hapa mnufaika akiwa ni mfanyabiashara yeye mwenyewe) lakini bado wafanyabiashara walichukua muda kuitia wito.Serikali iliweka mikakati ya kufuatilia utekelezaji na kuhusisha viongozi kuanzia ngazi ya taifa (Waziri), mkoa na wilaya. Tumewahi kuona wakati mwingine serikali ikiweka hata bei elekezi mfano kwenye bidhaa kama mafuta n.k. 

Katika hili la kurudisha kodi kwenye bidhaa ya pedi, mimi naona serikali imetumia tathmini ya muda mfupi sana kuhitimisha kuwa kutolewa kwa kodi hii hakuwanufaishi walengwa. 

Mwaka mmoja ni muda mfupi sana, hasa pia kama hakukuwa na mikakati madhubuti kutoka ngazi ya taifa mpaka vijijini ya kuweka mpango kazi na washika dau wa kusimamia utekelezaji wa sera badala yake tukawaachia wafanyabiashara wenyewe wafuate agizo wakati inafahamika kuwa siku zote mfanyabiashara lengo lake la kwanza ni kutengeneza faida na si kunufaisha watu. 

Serikali ilikuwa na jukumu kubwa hapa kama mlinzi wa maslahi ya wananchi.Ilikuwa ni muhimu serikali iweze kushirikiana na washika dau kama ambavyo tumeona imefanya vizuri kwenye kusimamia utekelezaji wa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

Kuna wengine wanasema kodi iliyoshushwa katika viwanda kutoka asilimia 30 kwenda 25 itasaidia kwa sasa. Naomba niseme, Hapana. Tunahitaji misamaha yote ili kupata unafuu mkubwa zaidi. Ingawa kodi katika uzalishaji imeshushwa kwa asilimia tano (5) ijimradi kodi ya ongezeko la thamani (VAT 18%) bado itakuwepo, bado mlaji wa mwisho hatapata unafuu. Siku zote mlaji wa mwisho ndio hulipa kodi inayoongezwa kwa wafanyabiashara na hiyo itakuwa hivyo hivyo kwa kodi hii ambayo imerudishwa kwenye bidhaa za hedhi. Bei zitapanda maradufu

Bidhaa ya pedi haikutakiwa hata kuuzwa in the first place,hasa kwa watu kama wanafunzi. Pedi ni essential need, wanawake hawachagui kupata hedhi,kututoza kodi kwa kupata hedhi kila mwezi, kwa kweli sio jambo la kibinadamu. Kwa hiyo tukisema tuweke lense ya Jinsia, bidhaa hii haikutakiwa hata kuuzwa, sema kwa sababu ya choices, ni muhimu soko liwe na bidhaa nyingi tofauti ili walaji wachague wenyewe chapa wanazopenda. Ila kwa watu kama wanafunzi hasa wa vijijini, bado si sawa kwanza kwa hii bidhaa kupatikana kwa kununua. Walitakiwa wapate BURE. 

Utafiti uliofanywa na UNICEF unaonesha kuwa wasichana hukosa siku nne (4) hadi tano (5) kwa mwezi kutokana na hedhi na msichana mmoja (1) kati ya kumi (10) huacha shule kila mwaka kutokana na kukosa vifaa vya kujihifadhia wakati wa hedhi. 

Suluhisho la muda mrefu hapa ilikuwa zipatikane bure, na kutolewa kodi kulikuwa kunaanza kutupeleka kwenye unafuu huo. Niseme, wafanyabiashara wana jukumu la kimaadili (moral obligation) la kuhakikisha hawajinufaishi na jitihada za kupunguza makali kwa walaji wa mwisho. Ubepari umekuwa ni sababu kubwa pia inayomdidimiza mwanamke na mtoto wa kike, sababu wenyewe umejikita zaidi kwenye kupata faida na sio maendeleo ya watu.


Mapendekezo

1. Serikali ifute pendekezo la kurudisha kodi kwenye pedi, msamaha wa kodi uendelee kubaki kama ulivyopitishwa mwaka jana. Kurudisha kodi kwenye pedi ni kuendelea kumtoza msichana na mwanamke kodi kwa kupata hedhi ambayo si sawa kiubinadamu. 

2. Serikali na washika dau waweke mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuhakikisha bei inashuka kwa kuandaa mikutano na wafanyabiashara katika eneo hili na ikiwezekana kuwepo na muda elekezi wa namna ambavyo mpango kazi utafanyiwa kazi ili kuleta unafuu kwa walengwa

3. Serikali iangalie uwezekano wa kuweka bidhaa ya pedi kwenye list ya essential needs kwenye sheria ya kodi ili kuhakikisha unafuu wa bei ni endelevu na hautabadilika badilika kila wakati

4. Kuwepo na mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha pedi inakuwa ni bidhaa inayopatikana bure hasa kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanabaki shule na kusoma na kupunguza mdondoko kwa watoto wa kike kwenye kupata elimu.


By Rebeca Gyumi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...