Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda,
Tume ya Mipango Zanzibar na Ofisi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge Taanzania (MKURABITA) zitaendeleza azma yake
muhimu ya kuhamasisha urasimishaji wa Wafanyabiashara wadogo wadogo wa
Zanzibar ili kuzifanya biashara zao kutambulika kisheria.
Kwa kufanya hivyo kutawawezesha Wajasiriamali mbali mbali kufanya
biashara endelevu zinazowakomboa kiuchumi na kuepuka kufanya biashara
ya kimazoea zisizoleta tija.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Reli ameyasema hayo
alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA
iliyomtembelea Ofisini kwake Migombani ikiwa ni mwendelezo wa kukagua
shughuli zinazofanywa na Kamati hiyo visiwani Zanzibar.
Amesema kwa Zanzibar kazi za urasimishaji hufanyika kwa kushirikiana
na Ofisi za Wilaya na Halmashauri husika ambapo Wafanyabiashara
hupatiwa mafunzo maalum ya urasimishaji.
“Unapokuwa rasmi unaweza kupata mkopo kirahisi, ukipata mkopo pia kuna
uwezekanao wa biashara kukua na pato la Taifa pia huongezeka”
alifafanua Katibu Juma Reli.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara na ukuzaji masoko Khamis Ahmad
Shauri amesema jumla ya Wafanyabiashara wadogo 154 walipatiwa mafunzo
ya urasimishaji Unguja na Pemba kwa mwaka 2018/2019
Amefahamisha kuwa Wafanyabiashara wanaporasimishwa hupata fursa ya
kuweza kukopa Mitaji katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Benki ambayo
huwasaidia kuziendeleza biashara zao kwa faida yao na vizazi vyao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya MKURABITA Balozi
Daniel Ole Njolay ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupunguza gharama za uanzishwaji wa biashara kwa wananchi ikiwemo
ukataji wa Leseni ili kuyafanya mazingira ya biashara kuwa rahisi.
Mratibu wa MKURABITA Tanzania Dkt. Seraphia Mgembe ameiomba Wizara ya
Viwanda na Biashara Zanzibar kuandaa mijadala ya wazi kwa wananachi
walionufaika na MKURABITA Zanzibar ili iwahamasishe wananchi wengine
kurasimisha biashara na rasilimali zao.
Awali Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA walimtembelea Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Mwita M. Mwita na kufanya
mazungumzo naye ambapo aliwaeleza kuwa Ofisi yake tayari imeratibu na
kufanya utambuzi wa Viwanja zaidi ya 10,000.
Amesema baada ya utambuzi huo Serikali ya Mapinduzi ipo mbioni kutoa
hati za Viwanja hivyo kwa wananchi ili kufanya shughuli zao na kuepuka
migogoro ya ardhi.
Kamati hiyo pia ilipata fursa ya kutembelea Wajasiriamali walionufaika
na MKURABITA na kuona maendeleo yao ambapo pia walielezea changamoto
ya masoko kwa bidhaa wanazozizalisha.
Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Taanzania
(MKURABITA) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mwaka 2004 ikiwa ni mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini
Tanzania MKUKUTA na MKUZA ambapo walengwa hutumia raslimali na
biashara zao zilizorasmishwa katika kujipatia mitaji, soko na fursa
zingine.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Mwita M. Mwita (mwenye Mkoba) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA waliomtembelea ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Reli akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA iliyomtembelea Ofisini kwake Migombani ikiwa ni mwendelezo wa kukagua shughuli zinazofanywa na Kamati hiyo visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Biashara na ukuzaji masoko Zanzibar Khamis Ahmad Shauri akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa kurasimisha biashara ndogo ndogo Zanzibar kwa mwaka 2018/19 mbele ya Kamati ya Uongozi ya MKURABITA.
Mjasiriamali ambaye amepata mafunzo kutoka kwa MKURABITA Furaha Juma Abdalla akiwauzia bidhaa anazozalisha baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA waliomtembelea kwake Chukwani Zanzibar kujua maendeleo ya shughuli zake.
Mratibu wa MKURABITA Tanzania Dkt. Seraphia Mgembe akiangalia Mikoba
inayotengenezwa na Mjasiriamali Neema Betraham wa Kikwajuni mjini
Zanzibar mara baada ya kufika kuangalia shughuli za Wajasiriamali hao.
Picha na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...