Na Veronica Kazimoto

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbibo ametembelea bandari kavu ya Said Bakhresa (SSB-ICD) na African ICD ambapo amewataka Maofisa Forodha wa Mamlaka hiyo kuzingatia uwajibikaji, weledi na uadilifu wakati wote wanapotimiza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza na maofisa hao kabla ya kukagua mizigo iliyopo katika bandari hizo, Naibu Kamishna Mkuu huyo amesema kwamba, uzingatiaji wa maadili katika sehemu za kazi utasaidia kuondoa malalamiko na kero kwa walipakodi ambao ni wadau wakuu wa TRA.

“Jukumu la kujenga taswira ya mamlaka ni la kila mtumishi wa TRA. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anafanya kazi bila upendeleo, anawajali wateja ikiwa ni pamoja na kutumia lugha yenye staha, alisema Naibu Kaimshna Mkuu Mbibo.

Kwa upande wake Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Ben Usaje amewasisitiza watumishi hao kutojihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaichafua Mamlaka ya Mapato Tanzania.

“Sote humu ndani tunajua kuwa, kupokea au kutoa rushwa ni kinyume cha sheria ya nchi yetu na yeyote atakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Hivyo, hakikisheni mnaepuka kabisa vitendo hivyo vya rushwa kwani vitawasababishia kupoteza kazi na kufikishwa mahakamani”, alisema Usaje. 

Baadhi ya majukumu ya Ofisi za Forodha zilizopo katika bandari kavu hapa nchini ni kuhakikisha kuwa taratibu zote za kuingiza mizigo ndani ya nchi zinafuatwa pamoja na kuhakikisha kwamba kodi stahiki inalipwa na wenye mizigo kabla ya kutoa mizigo yao katika bandari hizo.
 Meneja wa Bandari Kavu ya African ICD, Abeid Said (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kuhusu bandari hiyo kwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbibo (wa pili kushoto aliyevaa tai ya mistali) wakati alipotembelea bandarini hapo.
 Afisa Forodha Mfawidhi wa Bandari Kavu ya African ICD, Brian Japheth akitoa maelezo juu ya mizigo iliyopo bandarini hapo kwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo (wa pili kulia) wakati alipoitembelea bandari hiyo. Kushoto kwake ni Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Ben Usaje.
 Afisa Forodha Mfawidhi wa Bandari Kavu ya Said Bakhresa (SSB-ICD), Caleb Mwangalaba akitoa maelezo mafupi kuhusu bandari hiyo kwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo (kushoto) wakati alipoitembelea bandari hiyo kuona jinsi inavyofanya kazi.
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo (aliyevaa tai ya mistali) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Forodha waliopo katika bandari kavu ya African ICD wakati alipoitembelea bandari hiyo. Kushoto kwa Naibu Kamishna Mkuu ni Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Ben Usaje na kulia kwake ni Naibu Kamishna wa Biashara na Uwezeshaji, Godfrey Kitundu.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...