Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifungua Ofisi na Tawi la Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe, wakati akifungua Ofisi na Tawi la Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifungua akaunti katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), baada ya kufungua Ofisi na Tawi la Benki, katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019. Kulia ni Ofisa Huduma kwa Wateja Elizabeth Mkondya. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihifadhi fedha baada ya kufungua akaunti katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), baada ya kufungua Ofisi na Tawi la Benki ya Benki hiyo, iliyopo katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019. Kushoto ni mtoa huduma wa fedha, Nasra Namkudai. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kufungua Ofisi na Tawi la Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ashantu Kijaji, wakati wa ufunguzi wa Ofisi na Tawi la Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), katika jengo la PSSSF jijini Dodoma.





*Ihakikishe huduma zake zinawafikia wananchi wa mijini na vijijini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta ya fedha inapaswa kuwa imara na kuhakikisha huduma zake zinawafikia wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini ili iweze kutoa mchango unaokusudiwa katika kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. 

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 24, 2019) wakati alipofungua Ofisi Ndogo na Tawi la Benki ya Biashara ya TIB jijini Dodoma. Amesema ukuaji wa sekta ya huduma za kifedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Waziri Mkuu amesema benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi, hivyo, benki zinatakiwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, kuwahamasisha na kuwaelimisha umuhimu wa kutumia benki. 

“Wananchi nao pia wana wajibu wa kuzitumia benki hizi kwa kutunza akiba zao na kukopa wakati wanapohitaji kuwekeza kwa malengo yaliyokusudiwa. Suala la msingi ni kuwa mnapokopa mkumbuke pia kurejesha kulingana na makubaliano.”

“Sifurahishwi sana na takwimu zinazoonesha kwamba ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania wote ndiyo wanaopata huduma za kifedha kupitia mifumo halali ya kibenki, huku asilimia 48.6 wakipata huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu na asilimia 35 ya waliosalia kutopata kabisa huduma rasmi za kibenki.”

Waziri amesema hali hiyo haikubaliki kwenye nchi kama Tanzania ambayo inakabiliana na ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ametoa wito kuwa benki zote ziendelee kubuni mikakati na mbinu zitakazowawezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki tena kwa gharama nafuu ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua kutoka kwenye umaskini. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema tozo za mabenki kwa wateja bado ni kubwa na haziwasaidii wananchi wa kawaida, kwa hiyo, zipunguzwe. “Riba kwa wakopaji nazo ziko juu sana ukilinganisha na mfumuko wa bei, pia nazo zipunguzwe.”

Kuhusu changamoto ya riba kubwa inayotozwa kwa mikopo ya benki, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imefanikiwa kupunguza riba ya hati fungani za Serikali, pamoja na ile inayotozwa kwa mabenki yanayokopa Benki Kuu. Moja ya lengo la kufanya hivyo ni kutaka riba za mabenki zipungue. 

“Naomba mabenki yaunge mkono jitihada hizo za Serikali kwa kupunguza riba zinazotozwa hasa kwenye mikopo ya watu binafsi na biashara ndogo ndogo kwani hawa wakipata unafuu wataweza kukuza biashara zao na hivyo kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji.”

Akizungumzia suala la baadhi ya benki kuwa na tawi moja au mawili jijini Dar-es-Salaam tu, Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuzitathimini upya benki za aina hiyo.

“Leo narudia tena kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuzisimamia benki zetu ili zifungue matawi yake hadi vijijini waliko wenye uhitaji.! Kwanini? benki nyingi zimejikita katika kutafuta faida pekee bila kuwekeza kwa faida ya nchi yetu? Hadi sasa tuna benki ambazo zimekuwa siku zote na tawi moja tu tena liko Dar-es-Salaam. Benki Kuu ya Tanzania isisite kuchukua hatua za kisheria kurekebisha hali hiyo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya TIB, Frank Nyabundege amesema kwa kipindi cha miaka minne benki hiyo imeweza kukuza mtaji kutoka sh. bilioni 206 wakati inagawanywa mwaka 2015 mpaka kufikia sh. bilioni 409 mwishoni mwa mwaka 2018 sawa na ukuajia wa aslimia 98.5.

Mkurugenzi huyo amesema mbali na kufanikiwa katika kukuza mtaji, pia benki hiyo imeweza kukuza amana za wateja kutoka sh. bilioni 110 mwaka 2015 mpaka sh. bilioni 338 mwezi Disemba 2018, sawa na ukuaji wa asilimia 207.

“Mafanikio mengine yabenki ya TIB katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na kuanza kutengeza faida angalau ya sh. bilioni 1.3 mwaka jana (2018), kutoa mchango stahiki katika Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha sh. milioni 250.”

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa benki hiyo imetoa mikopo na dhamana kwa taasisi za umma hadi kufikia shilingi bilioni 224.35 kwa kipindi kilichoishia Machi 2019, kulipa kodi Serikalini kiasi cha sh. bilioni 19.2 tangu benki ianzishwe na kutoa mikopo kwenye sekta ya viwanda jumla ya sh. bilioni 65.12.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...