Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo Prof. Mohammed Janabi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuisaidia Taasisi hiyo kupata jengo la Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto.

Prof. Janabi amesema mwisho mwa wiki kwamba kufuatia maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli aliyoyatoa mapema mwaka jana (2018), moja ya majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili lililopo jirani na Taasisi hiyo lilikabidhiwa kwa Taasisi hiyo na Serikali ikatoa fedha za kulikarabati na kuwekewa miundombinu ya kutolea huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

Ameongeza kuwa jengo hilo lina lina vitanda 40 vya kawaida na vitanda 8 vya watoto wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na kwamba kukamilika kwake kutaiwezesha Taasisi hiyo kupata vyumba vipya 4 vya kliniki ambavyo vitawawezesha Madaktari kuwaona watoto 60 kwa siku.

Prof. Janabi amebainisha kuwa kabla ya kupatiwa jengo hilo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ililazimika kuwachanganya watoto na watu wazima katika sehemu moja iliyojumuisha chumba cha ICU, wodi na pia kliniki ambayo iliwawezesha Madaktari kuona wagonjwa kati ya 25 na 30 tu kwa siku.

"Kwa furaha kubwa kabisa, mwezi uliopita jengo letu limekwisha kama unavyoliona lina vitanda 40 kwa ajili ya watoto tu, lina vitanda 8 kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watoto tu na muda wowote kuanzia sasa tutalifungua.

"Sasa nini faida kubwa ambayo tutaipata sisi kama Madaktari, sasa hivi watoto wagonjwa wakitoka chumba cha upasuaji (Theatre) watakwenda moja kwa moja kwenye ICU ya watoto, hii ni tofauti na hali ilivyokuwa kwenye hili jengo kubwa tulilokuwepo ambapo Daktari alikuwa anaingia wodini anamuona mgonjwa wa kwanza mtu mzima ana kilo 90, kitanda kinachofuatia kuna mtoto ana kilo 5 ambaye pia tumemfanyia upasuaji, kwa hiyo uwezekano wa kufanya makosa ulikuwa mkubwa sana iwe kwenye kutoa dawa au huduma nyingine. Ndio maana tunamshukuru sana Mhe. Rais Magufuli kwa kutusaidia na ufanisi wetu wa kazi utakuwa mkubwa zaidi" amesema Prof. Janabi.

Aidha, Prof. Janabi amewashukuru wadau binafsi waliochangia ukarabati wa jengo hilo wakiwemo Jumuiya ya Kihindi ya BAPS na Benki ya CRDB waliofanikisha kukamilika kwa jengo hilo. Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani amesema tatizo la magonjwa ya moyo hapa nchini ni kubwa ambapo katika kila watoto 100 wanaozaliwa 1 ana tatizo la moyo hivyo kujengwa kwa jengo hilo kuna umuhimu mkubwa kwa Watanzania ambao awali walikosa huduma ama kulazimika kwenda nje ya nchi.
 Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Dkt. Naiz Majani akisimamia upimwaji wa mtoto ndani ya jengo la Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto cha taasisi hiyo ambalo lilitolewa mwaka jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Jengo hilo ambalo limemalizika kukarabatiwa mwezi uliopita na tayari limeshaanza kupokea wagonjwa, lina vitanda 40 kwa ajili ya watoto tu, na pia lina vitanda 8 kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watoto tu na muda wowote kuanzia sasa litafunguliwa rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo Prof. Mohammed Janabi akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto katika taasisi hiyo ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani wakibadilishana mawazo nje ya jengo la Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto cha taasisi hiyo ambalo lilitolewa mwaka jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Jengo hilo ambalo limemalizika kukarabatiwa mwezi uliopita na tayari limeshaanza kupokea wagonjwa, lina vitanda 40 kwa ajili ya watoto tu, na pia lina vitanda 8 kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watoto tu na muda wowote kuanzia sasa litafunguliwa rasmi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...