Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza umuhimu wa Sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya moja, wakati akifungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019. 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa, akitoa hotuba wakati wa mkutano wa kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza umuhimu wa Sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya moja, wakati akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019. 
Mratibu wa Dawati la Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka (wa kwanza kulia) akiwa katika chumba maalum cha Menejimenti ya Taarifa za zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019. 

************************************* 



Kufuatia nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, Tanzania kwa kushirikiana na Kenya wameanza kutekeleza zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, lilofunguliwa leo mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga, kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu. 

Zoezi hilo, linazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla ya washiriki 150 ambao wanatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo. 

Akiongea leo tarehe 11 Juni, 2019, wakati wa Kufungua rasmi zoezi hilo la siku nne, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amefafanua kuwa, serikali kupitia Wizara hiyo inatumia zoezi hilo kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko. 

“Hapa nchini Tanzania tunalo Dawati la Kuratibu masuala ya Afya Moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati hilo sisi kama wizara ya Afya tunasubiri tu ripoti ya zoezi hili na tutaitekeleza mara moja. Utekelezaji wa ripoti hiyo tutahakikisha unakuwa wa ufanisi na tija kwa nchi ili tuweze kusaidia kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya hapa nchini kwa kuzingatia dhana ya Afya moja.” Amesisitiza Waziri Ummy. 

Aidha, Waziri Ummy, ameongeza kuwa zoezi hilo linalenga kutathmini utaratibu wa kutumia kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini pia kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika, kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro. 

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi hiyo, itaendelea kuratibu sekta zote za Afya nchini kwa kutumia Dhana ya Afya moja, ili kuhakikisha Afya za wananchi zinakuwa imara na salama kwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababisha maafa. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina, amebainisha kuwa, kwa kutambua umuhimu wa Dhana ya Afya moja, Wizara inafahamu kuwa mifugo huwa ni chanzo cha vimelea vya magonjwa ambayohuambukizwa binadamu,hivyo serikali imeendelea kuboresha maabara za Mifugo nchini ili kuweza kutambua vimelea kwa haraka na wakati ili visisababishe magonjwa ya mlipuko kwa binadamu. 

Naye, Waziri wa Afya wa Kenya, Mhe. Sicily Kariuki, amebainisha kuwa zoezi hilo ambalo linahusisha mlipuko wa virusi vinavyo shabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya, kwa kuwa washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwakuzingatia Dhana ya Afya Moja. 

Zoezi hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga. 

Zoezi hilo ambalo linafanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, linaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...