Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
THAMANI ya mali  zilizotaifishwa kutokana na uhalifu zimefikia shilingi bilioni 93.16. Mali  hizo ni pamoja na madini, nyumba, magari, fedha za upatu, mbao na maliasili zilitaifishwa kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2019 zikitokana na uhalifu wa kupangwa, utakatishaji fedha, kughushi na wanyamapori.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan  wakati  akifungua maadhimisho ya miaka 10 ya Umoja wa taasisi zinazokabiliana na uhalifu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (ARINSA) ambapo amesema kuwa miongoni mwa mali walizotaifisha ni madini yenye thamani ya Shilingi bilioni 32.

Amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na marekebisho makubwa katika sheria za nchi ikiwemo Sheria ya Utakatishaji wa mali zinazotokana na Uhalifu na Sheria ya Kuzuia Utakatishafi wa Fedha Haramu ili kuhakikisha zinakuwa na ufanisi unaotakiwa katika kupambana na mbinu mpya za kihalifu hasa unaovuka mipaka.

Samia ameeleza kuwa  kuwepo wapelelezi na waendesha mashitaka wachache waliopata mafunzo kupitia umoja huo, wamechangia kutaifishwa kwa mali hizo kutokana na ujuzi walioupata.

Makamu wa Rais amesema kuwa utekelezaji na kasi ya Rais Magufuli unaendana sana na malengo ya ARINSA hasa katika kukemea masuala ya rushwa, ufisadi na kujilimbikizia mali.

Amesema kuwa umoja huo umetanua wigo wa ushirikiano katika masuala ya upelelezi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za kiupelelezi zinazosaidia kuharakisha kukamilika kwa maombi ya ushahidi nje ya nchi na upatikanaji wa mali zinazohusiana na uhalifu.

Makamu wa Rais amesema kuwa makosa mengi ya kupangwa na mbinu za utendekaji wake wa kisasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia hususani Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kueleza kuwa programu za wapelelezi na waendesha mashitaka wameweza kujengewa uwezo kwenye makosa ya kifedha, wanyamapori na misitu na ufadhili wa ugaidi ikiwa ni pamoja na kufuatilia mali walizozipata wahalifu au kuzitumia kutenda uhalifu ili kuzitaifisha.

Aidha amesema kuwa  nchi wanachama zimefaidika kupitia programu za mafunzo kwa kurekebisha sheria  mbalimbali zilizokuwepo na kutunga sheria mpya ili kurahisisha utaifishaji na urejeshaji wa mali zinazohusiana na uhalifu na kuhakikisha nchi zinaendelea kuwa salama.

Vilevile amezishauri nchi wanachama kuwa kila nchi itakapotaifisha mali asilimia fulani ya fedha ipelekwe kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka na baadaye kuja katika taasisi hiyo ili iweze kujitegemea kifedha.

Kwa upande wake, Rais wa ARINSA, Biswalo Mganga ambaye pia ni Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) amesema kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2019 umoja huo umeweza kutaifisha mali zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.406. amesema kiwa mwaka huu pekee mali zilizotaifishwa zina thamani ya Dola za Maarekani milioni 700 na kwamba mali zinazoshikiliwa zinathamani ya Dola za Marekani 594.23 na maombi ya kutaifisha mali ni 142.

Amesema changamoto wanazokabiliana nazo ni kupoteza thamani ya mali zinazokamatwa na kukaa muda mrefu kwenye vituo vya polisi  na baadhi zinaharibiwa na wahalifu wenyewe zikiachwa mikononi mwao.

 Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ametumia wasaa huo kutangaza utalii wa ndani hasa mlima kilimanjaro na kusema kuwa ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii hauwezi kutimia endapo hakuna amani kwa watu na mali zao kwenye nchi wanachama.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi wanachama 16 ambazo ni; Tanzania, Lesotho, Malawi, zambia, Botswana, Afrika kusini, Eswatini, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Angola, Madagascar, Msumbiji, Mauritus, Namibia na Shelisheli.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan(katikati) akiwa katika Mkutano wa Umoja wa Urejeshaji wa Mali zinazohusu uhalifu uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo , ARINSA pia walifanya maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwake 2009,kutoka kulia ni Mkuu wa Mpango wa Kuzuia Utakatishaji Fedha, Michiel Van Dyk, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP) Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Augustine Mahiga, Kushoto ni Jaji Dkt.Eliezer Mbuki Feleshi, na Mshauri wa UNOC, Fitz Ray Drayton.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...