Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
WAANAWAKE wawili wakazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kujipatia mkopo wa Sh milioni 25 kwa njia ya udanganyifu.

Washitakiwa hao ni Veronica Tembe (45) na Lilian Kisamo (41) wote wakazi wa Tegeta.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile kuwa katika siku na mahali pasipojulikana  washitakiwa wote kwa pamoja walikula njama ya kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.

Nguka alidai katika mashitaka ya pili kuwa siku na mahali pasipojulikana mshitakiwa Tembe  akiwa na nia ovu alighushi kadi ya gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba za usajili T 504 BBT kwa madhumuni ya kuonesha kuwa kadi hiyo ni halisi na imetolewa na Mamlala ya Mapato Tanzania (TRA).

Pia inadaiwa Novemba 27, 2012 katika Benki ya EFC Tanzania Microfinance Ltd iliyopo Victoria ndani ya Wilaya ya Kinondoni,  Tembe aliwasilisha kadi hiyo ya kughushi kwa maofisa wa EFC ili aweze kupatiwa mkopo.

Katika mashitaka ya nne, mshitakiwa Tembe anadaiwa aligushi leseni ya biashara kwa madhumini ya kuonesha kuwa leseni hiyo imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Nguka aliendelea kudai kuwa, Novemba 27, 2012 huko EFC Microfinance Ltd iliyoko eneo la Victoria, mshitakiwa aliwasilisha leseni ya biashara ya kughushi kwa Ofisa wa benki ya EFC kwa madhumuni ya kuonesha kuwa leseni hiyo imetolewa na Halmashauri ya manispaa ya Ilala huku akijua kuwa siyo kweli.

Inadaiwa  siku na mahali hapo mshitakiwa Tembe  akiwa na nia ovu alijipatia mkopo wa Sh milioni 25 kupitia akaunti yake  iliyopo katika benki hiyo kwa njia ya udanganyifu akijifanya kuwa yeye ndiye mmiliki wa leseni ya biashara na leseni hiyo ya gari ambavyo vilikuwa kama dhamana ya mkopo huo huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika mashitaka ya saba, inadaiwa  mshitakiwa Tembe alitakatisha Sh milioni 25 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi.

Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka hayo na mshitakiwa Kisamo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti huku mshitakiwa Tembe alirudishwa rumande kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana.

Hakimu Rwizile aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 2, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upelelezi bado haujakamilika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...