WATUMISHI saba wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, kwa tuhuma za kukutwa na vitambulisho vya taifa vipatavyo 15,000.
Mbali ya vitambulisho hivyo, watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa, pia wamekamatwa na kompyuta mpakato mbili, meza, ‘scanner’, kamera, steshenari, maturubai, BVR kits, friji ndogo na vitu mbalimbali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, ACP Wankyo Nyigesa, amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba tukio hilo limetokea wakati wa kuhamishwa kwa vifaa vya wakala huyo kutoka ofisi za awali eneo la TANITA, kwenda ofisi mpya zilizoko Tamko.
“Watumishi hao saba, kati yao wanaume sita, mwanamke mmoja, wamefanya tukio hilo wakati wanatoa vifaa hivyo Tanita ofisi ya zamani, kuhamia ofisi mpya ambapo wakiwa njiani waliiba vitu hivyo kisha kuviuza,” alisema Kamanda Nyigesa.
Ameongeza kwamba baada ya tukio hilo uongozi wa NIDA ukatoa taarifa Polisi Juni 14 kuhusiana na tukio hilo, na kwamba katika kufanikisha azma yao walitumia gari ndogo aina ya Toyota Spacio yenye namba za usajili T 365 DFS.
“Jeshi la Polisi lilifuatilia gari hiyo iliyokuwa imebeba jenereta ambayo walikuwa wanakwenda kuiuza, baada ya watumishi hao kupekuliwa majumbani mwao walikutwa na vifaa vya ofisi ambavyo ni kompyuta mpakato mbili, nyaya za kompyuta na boksi moja lenye vitambulisho hivyo,” alisema Kamanda Nyigesa.
Aliongeza kwamba vitu vilivyoibiwa vya NIDA vyote vina thamani ya Tsh. Milioni 15, huku akiwaomba watumishi wa umma na taasisi na mashirika watu binafsi kuwa watiifu wanapokabidhiwa mali za umma wazichunge kama mboni ya jicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...