Na Francis Godwin, Iringa
Diwani kata ya Mwangata jimbo la Iringa mjini Nguvu Chengula alazimika kuwapigia magoti viongozi na wanachama wa vikundi vya wajasiliamali vya umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kata ya Mwangata kuwaomba kutorudia makosa ya usaliti waliyoyafanya mwaka 2015 ya kuchagua viongozi wa upinzani na kuomba sasa wachague viongozi wa serikali za mitaa pia madiwani ,wabunge na Rais Dkt John Magufuli mwaka 2020.
" Naomba kuwaomba sana tena sana ninyi wanachama na viongozi wa UWT kata ya Mwangata tuepuke usaliti wakati wa uchaguzi simamieni na waelimisheni wananchi wachague viongozi wanaotokana na CCM ili kuleta heshima kwa chama ...kwanza naomba kuwapigia magoti kabisa maana naomba kutoka moyoni chagueni CCM " alisema Chengula huku akiwa amepiga magoti
Diwani huyo aliyasema hayo alifikia uamuzi huo wa kuwapigia magoti wanavikundi hao jana katika ukumbi wa Damu ya Yesu wakati wa uzinduzi wa vikundi nane vya ujasiliamali vya umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kata ya Mwangata .
Alisema kuwa sehemu kubwa vikundi ndani ya Manispaa ya Iringa havijafikiwa na mikopo hiyo kutokana na uamuzi wa wananchi walioufanya mwaka 2015 kwa kuchagua madiwani wa upinzani na mbunge wa upinzani ambao wamekuwa hawashughuliki na kero za wananchi zaidi ya kujitazama wao hivyo njia pekee ni kutorudia makosa kwenye uchaguzi wa serikali ya mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2020 kuhakikisha wanachagua viongozi watokanao na CCM pekee.
Aidha aliitaka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutoa mikopo inayopaswa kutolewa kupitia makusanyo yake ya ndani ya kwa vikundi vya wajasiliamali wa kata ya Mwangata ili kuwawesha kukuza mitaji yao kwani lengo la serikali kuagiza Halmashauri kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake ,vijana na walemavu ni kuwawezesha kupanua wigo zaidi ya shughuli zao .
Diwani Chengula alisema kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo kusajiliwa katika Halmashauri tayari mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Rose Tweve ( CCM) amevitembelea vikundi vya kata ya Mwangata na kuvisaidia fedha kiasi cha shilingi 500,000 kwa ajili ya kukuza mitaji huku yeye kama diwani wa kata ameviongeza kiasi cha shilingi 800,000 ili kuviongezea nguvu ya kusajiliwa kisheria.
“ Serikali ya chama cha mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wetu Rais Dkt John Magufuli ipo kuona wananchi wenye sifa ya kupewa mikopo hii wananufaika nayo na mikopo hii haitakiwi kurejeshwa kwa riba yoyote hivyo ni haki ya kila mwenye sifa kupewa mikopo hiyo iwapo atakuwepo kwenye kikundi “ alisema Chengula.
Hivyo alisema fedha hizo ni haki ya makundi husika na lazima Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutoa mikopo hiyo kwa makundi hayo bila kuwepo kwa ubaguzi wowote iwapo vikundi vitakuwa vimetimiza sifa zinazohitajika .
“ Mimi kama diwani wenu nitahakikisha napambana kuubana uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa ili fedha hizo ziweze kutolewa kwa vikundi vyote ambavyo vitakuwa vimetimiza sifa ya kupewa mikopo hiyo na sitakubali kuona mnahangaika kutafuta mitaji wakati fedha za serikali zipo “ alisema Chengula
Kuwa vikundi vya kata hiyo vimekuwa mfano wa vikundi vingine ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutokana na aina ya shughuli za uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji batiki na vikapu vya kisasa ambavyo wanachama wake wamekuwa wakifanya na shida yao ni mitaji ya kuboreshea huduma zao.
Naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Joseph Ryata alisema kuwa uhakika wa vikundi hivyo kupewa mikopo upo na kutaka kukamilisha taratibu za usajili wa vikundi hivyo hasa vile ambavyo havijasajiliwa .
Aidha alisema wajibu wa halmashauri hiyo kuendelea kuwaunganisha wananchi wake na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo nafuu kama inayotolewa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) mkoa wa Iringa .
Awali wanavikundi hao wakitoa changamoto zao wakati wa kikao hicho cha uzinduzi wa vikundi vya vya wajasiliamali kata ya Mwangata walisema changamoto kubwa ni Halmashauri kushindwa kutoa mikopo kwa wakati .
Diwani wa kata ya Mwangata katika Halmashauri ya manispaa ya Iringa Nguvu Chengula akiwa amepiga magoti kuomba wanachama wa vikundi vya ujasiliamali vya umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kata ya Mwangata kusaidia CCM kushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa jana wakati wa uzinduzi wa vikundi hivyo ukumbi wa damu ya Yesu Mwangata (Picha na Francis Godwin)
Diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengulla akionyesha fedha kabla ya kuwakabidhi wanavikundi kwa ajili ya usajili wa vikundi
Diwani wa kata ya Mwangata Nguvu Chengulla akikabidhi fedha wanavikundi kwa ajili ya usajili wa vikundi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...