Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile akikagua dawa na vifaa vinavyotumika katika kutibu mgonjwa wa Ebola, kulia ni Dkt. Praygod Swai wa Zahanati ya Bangwe iliyotengwa maalum kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa Ebola akimuonesha vifaa hivyo. Hema lilotengwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa Ebola katika bandari ndogo ya Kibirizi ikiyoko mkoani Kigoma.Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akipimwa joto la mwili na mhudumu wa uwanja wa ndege mara baada ya kufika katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akimpima joto la mwili mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw. Samson Anga wakati alipotembelea bandari ya Kigoma kuona hali ya utayari wa mkoa huo katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akioneshwa vifaa vya kujikinga na Ebola kutoka kwa mhudumu wa afya wa bandari ndogo ya Kibirizi Mkoani Kigoma wakati wa ziara yake mkoani humo kuangalia utayari wa mkoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile (Kulia) akitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Paul Chaote jinsi ya kuweka vifaa na kupangiliana hema (Isolation centre) kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Samson Anga. 
…………………….. 
Na WAJMW-Kigoma 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo ametembelea baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma kuona utayari wa mkoa huo katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. 
Dkt. Ndugulile ametembelea maeneo ya Bandari kuu ya Mkoa, Uwanja wa ndege, bandari ndogo ya Kibirizi na Zahanati ya Bangwe ambayo imetengwa maalumu kwa ajili ya kutoa matibabu kwa mtu atakayebainika kuwa na virusi vya Ebola. 

Naibu Waziri ameonekana kutoridhishwa na utayari wa Mkoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini huku akiitaka timu iliyoandaliwa chini ya Mkuu wa Wilaya Samson Anga na Mganga Mkuu wa Mkoa Paul Chaote kuendelea kutoa mafunzo kwa timu iliyoandaliwa jinsi ya kujikinga na kutoa huduma kwa mgonjwa atakayebainika. 

“Hatuna mgonjwa wa Ebola ndani ya nchi, lakini kutokana na hali ya ugonjwa huu katika nchi jirani kuna umuhimu wa sisi kama nchi kuendelea kujipanga na kuhakikisha kwamba mifumo yetu yote imekaa vizuri kipindi mgonjwa atakapojitokeza, hivyo nakuomba Mkuu wa Wilaya na Mganga Mkuu wa mkoa kuendelea kusimamia hili”. Amesema Dkt. Ndugulile. 

Mapungufu aliyobaini Dkt. Ndugulile ni pamoja na wahudumu kutozingatia kanuni walizofunzwa juu ya kujikinga na maambukizi pindi watakapokua wakihudumia mgonjwa, kutokua na vifaa vya kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola kama vitanda kwenye vituo vya Isolation na watumishi kutokua na uelewa na utayari wa kutosha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu. 

Dkt. Ndugulile yupo Mkoani Kigoma kwa ziara ya siku tatu ambapo pamoja na maeneo mengine atatembelea mpaka wa Manyovu ili kuona hali ya utayari ya mpaka huo kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na kisha atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...