Jumuiya ya Madola imeonesha kuridhishwa na namna Tanzania inavyotekeleza mageuzi ya kiuchumi,uwajibikaji na uawala bora kwa wananchi wake jambo ambalo jumuiya hiyo inalihimiza na kulisimamia kwa Nchi wanachama wake.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi za sekretarieti ya jumuiya hiyo zilizopo London Nchini Uingereza.

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland ameeleza kuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Prof. Palamagamba John Kabudi kuhusu utekelezaji wa masuala ya demokrasia,utawala bora na utawala wa sheria pamoja na Haki za binadamu nchini Tanzania na kwamba Jumuiya hiyo inatambua juhudi hizo na inaunga mkono hatua hiyo.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa mbali na kuhimiza utekelezaji wa utawala bora,haki za binadamu na utawala wa sheria pia Jumuiya ya Madola imelenga kukuza na kuwezesha biashara miongoni mwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo kupitia shirika la biashara la kimataifa (WTO) na mashirikiano ya biashara ya kikanda. 

Amesema ni jukumu la nchi za Jumuiya ya Madola kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika jumuiya hiyo ili kuiwezesha kupiga hatua za haraka za kimaendeleo na kuifanya Jumuiya nzima kuendelea bila ya kuacha nchi nyingine nyuma kutokana na uwepo wa migogoro ama machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa wanachama wa Jumuiya. Katika hili ameisifia Tanzania kwa kuwa na Amani na utulivu muda wote na pia kushiriki katika juhudi za kutatua migogoro kwa nchi zingine wanachama na wasio wanachama wa Jumuiya.

Kuhusu suala la mabadiliko ya tabia nchi,Katibu Mkuu huyo wa jumuia ya madola amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi. Ameeleza kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika program mbalimbali zinazolenga kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na masuala ya mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. palamagamba John Kabudi amemhakikishia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuwa Tanzania inaipa umuhimu mkubwa jumuiya hiyo na itaendelea kushirikiana nayo katika masuala ya ukuzaji wa uchumi, utawala bora hususani wakati huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi ya kiuchumi katika kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Ameipongeza jumuiya ya madola kwa mpango maalum inayoandaa kwa ajili ya kukuza na kuongeza biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo kwa ujumla jambo ambalo litafungua fursa biashara na masoko kwa bidhaa na mazao ya Tanzania. Amemuahidi Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania itashiriki ipasavyo katika mpango huo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kabudi pia amekubaliana na Bi Scotland kuangalia namna ya kuwasaidia vijana kuongeza ubunifu ili waweze kujiajiri na kuimarisha uchumi ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana huku akimpongeza Katibu Mkuu huyo kwa mageuzi makubwa anayoyafanya ndani ya jumuiya hiyo ili iweze kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi zaidi.

Profesa Palamagamba John Kabudi yuko London Nchini Uingereza kwa ziara ya siku nne kuhudhuria mkutano wa Mawaziri wa mambo ya Nje wa Jumuiya ya madola pamoja na mkutano wa Kimataifa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.
 Katibu Mkuu wa jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipomtembelea katika ofisi za Sekretarieti za jumuiya hiyo zilizopo London,Uingereza. Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro. July 9, 2019.
 Katibu Mkuu wa jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland akisalimiana na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika ofisi za Sekretarieti za jumuiya hiyo zilizopo London,Uingereza. July 9, 2019. 
  Katibu Mkuu wa jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika ofisi za Sekretarieti za jumuiya hiyo zilizopo London,Uingereza. July 9, 2019
 Katibu Mkuu wa jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika ofisi za Sekretarieti za jumuiya hiyo zilizopo London,Uingereza. July 9, 2019. 
 Katibu Mkuu wa jumuiya ya Madola Bi. Patricia Scotland akimsindikiza mgeni wake ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipomtembelea katika ofisi za Sekretarieti za jumuiya hiyo zilizopo London,Uingereza.July 9, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...