Muonekano wa barabara zilizojengw kupitia fedha za Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wilayani Temeke. 

Ujenzi wa soko kisasa linalojengwa Jijini Dar es Salaam kwa ufadhhili wa mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.



Na. Lilian Lundo - MAELEZO.

Jiji la Dar es Salaam ni kati ya majiji sita yaliyoko nchini Tanzania, likiwa Jiji la kwanza lenye idadi kubwa ya watu, ambapo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ilikuwa na watu 4,364,541 kati ya watu 44,928,923 nchi nzima. 

Kutokana na wingi huo wa watu, Jiji hilo limekuwa na changamoto nyingi kama vile foleni za magari, miundo- mbinu hafifu pamoja na baadhi ya maeneo kuathirika na mafuriko katika kipindi cha mvua.

Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na Mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ipo katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu katika Jiji hilo, ujenzi unaofanyika kwa mafungu kumi ambao ujenzi huo ulianza rasmi mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Ujenzi unaofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Jiji ambazo zinajengwa sambasamba na mifereji ya maji , taa za barabarani za sola, madaraja, masoko ya kisasa ambayo pia yatakuwa na huduma za kibenki pamoja na vyoo vya umma.

Akizungumza kuhusu mradi huo, mratibu wa DMDP Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Mhandisi Mkelewe Masalu Tungaraza amesema ujenzi wa miundombinu unaendelea ambapo mpaka sasa kuna barabara ambazo ziko katika hatua za ukamilishaji kama vile barabara za kuzunguka stendi za Makumbusho na barabara za Shekilango, Sinza

"Tunataka mtu akiwa Dar es Salaam aweze kuchepuka kwenda barabara nyingine, ili kupunguza foleni katika barabara kubwa.Vile vile, taa zitakazojengwa katika barabara hizo zitaimarisha usalama katika maeneo yanayozungukwa na barabara hizo," amesema Mhandisi Tungaraza.

Ameendelea kusema, barabara zitakazojengwa ni suluhisho kubwa kwa maeneo ambayo yalikuwa yanakumbwa na mafuriko kwani barabara hizo zinajengwa sambasamba na mifereje ya maji ya mvua na madaraja kwa maeneo ambayo ni sumbufu.

Mhandisi Tungaraza ametaja maeneo ambayo yatajengwa vyoo vya umma kwa Wilaya ya Kinondoni kuwa ni Tandale, Mburahati na Mwananyamala, ambapo uanishaji wa maeneo hayo umetokana na uhitaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa maeneo husika.

Kwa upande wa Mchumi wa Manispaa ya Ubungo, George Maiga amesema mradi wa DMDP unatarajia kujenga soko kubwa na la kisasa Mburahati kwa gharama ya shilingi bilioni. 2.079 ambapo itahusisha Jengo Kuu, eneo la Mama na Baba Lishe, Maliwato, eneo la wafanyabiashara wadogo wadogo , maduka, benki, machinjio ya kisasa na maduka ya kisasa.

"Ujenzi wa masoko haya umetokana na ongezeko kubwa la watu Jijini Dar es Salaam hivyo kusababisha kuzuka masoko mengi yasiyo rasmi katika mitaa," amesema Maiga. Amesema katika gharama hiyo ya mradi, Serikali imetoa shilingi milioni 900 ambayo ilitolewa ili kukamilisha mradi huo badala ya kwenda kukopa benki.Ameeleza kuwa, mara soko hilo litakapokamilika litaongeza mapato ya Halmashauri na wafanyabiashara wadogo wadogo watapata eneo la uhakika la kufanyia biashara.

Aidha, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kijichi, Manispaa ya Temeke, Anaclet Hayuka amesema soko linalojengwa Kijichi litakuwa na huduma zote muhimu pamoja na ofisi za maafisa Afya ili kufanya ukaguzi wa bidhaa mara kwa mara."Miaka mitatu ya utawala wa Rais Magufuli wananchi wameanza kuona cheche za maendeleo kupitia mradi wa DMDP," amesema Hayuka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...