Na Charles James, Michuzi TV

LICHA ya Serikali kuweka adhabu kali dhidi ya watu wanaowasababishia ujauzito wanafunzi na watoto waliochini ya umri wa miaka 18, lakini bado tatizo la mimba za utotoni ni kubwa huku mila na desturi zikitajwa kuchangia tatizo hilo hapa nchini Tanzania.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe Mwita Waitara, wakati wa maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani, yaliyoenda sambamba na uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya watu Duniani, tukio lililofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri Waitara amesema tatizo hilo ni kubwa kwa shule za msingi na sekondari ambapo ni asilimia 29 na limekua likichangiwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi, uendeshaji wa kesi ya kumtia mtu hatiani aliyempa mimba wanafunzi.

“Kuna mila na desturi ambazo watoto wa kike wakifikia umri fulani wanapewa chumba hivyo huko mtaani usiku kucha huwezi jua kinachoendelea, mazingira magumu ya usomaji.

“Hata katika uendeshaji kesi hizi mpaka kumtia mtu hatiani bado ni changamoto sana kwa kuwa wanaofanya vitendo hivyo wengine ni watu wa karibu na familia na wengine wanarubuni ndugu na kumalizana kimya kimya,”amesema Waitara.

Aidha licha ya hayo amesema uelewa wa watoto bado ni mdogo huku mimba nyingi zinazoripotiwa zimekua zikiishia hewani bila kujua mwisho wa kesi hiyo.Amesema wao kama serikali wanafanya vikao na wazazi mara kwa mara ili kuondokana na tatizo hilo, lakini bado mwitikio ni mdogo sana katika kudhibiti vitendo hivyo.

Kadhalika, amesema bado kuna changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi ambapo kati ya vizazi hai 100,000 watu 556 huripotiwa kufariki dunia kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni. 

“Nchi yetu ni moja ya mataifa 179 yaliyokutana nchini Cairo na tulikubaliana kutekeleza Mpango kazi tuliopanga katika Mkutano huo wa Idadi ya watu na maendeleo, serikali ya Tanzania imetekeleza mambo mengi, ni wajibu wetu kushirikiana kumaliza vifo vinavyotokana na uzazi na mimba za utotoni ili kila kijana atimize ndoto zake,”amesema.

Pia amebainisha kuwa serikali imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo na inalenga kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 hivyo ni lazima wahakikishe wanatokomeza tatizo hilo.

Kwa upande wake afisa kutoka UNFPA, Samwel Msokwa, akisoma taarifa ya idadi ya watu duniani iliyotolewa na Shirika hilo, amesema kadri watu wanavyoongezeka changamoto nazo zinaongezeka ambapo katika ripoti hiyo inaonesha tatizo la mimba za utotoni duniani bado ni kubwa sana.

“Ripoti inaeleza kinaga ubaga kuwa kuna tatizo la ukatili wa kijinsia licha ya taasisi mbalimbali kufanyiwa kazi, tuelekeze nguvu kukabiliana na tatizo hili,”amesema.

Naye, Mwakilishi wa Mkazi wa Umoja wa Mataifa(UN), Alvaro Rodriguez amesema vifo vinavyotokana na uzazi bado ni changamoto hasa kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15-19.
Naibu Waziri TAMISEMI, Mwita Waitara (katikati) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (kulia) na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa,  Alvaro Rodriguez wakiwa na vitabu vyenye ripoti yenye taarifa ya idadi ya watu Duniani iliyotolewa na Shirika la UNFPA.
 Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Idadi Duniani. 

 Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya idadi duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...