Na Karama Kenyunko, Michuzi TV.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kuwakamata raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka nyara Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu MO.

Hati hiyo ya kukamatwa imetolewa dhidi ya washitakiwa Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kudai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi dhidi ya mshtakiwa Mousa Twaleb anayedaiwa kumteka mfanyabiashara huyo, leo Julai 23, 2019 imekuja kwa ajili ya kutajwa na pia wameomba hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao wanatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo.

Wakili wankyo amedai kuwa, washitakiwa hao wataunganishwa katika kesi hiyo kujibu mashitaka mawili ya  kumteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari na kuongoza genge la uhalifu.

Mshitakiwa Twaleb ambaye ni dereva taksi na Mkazi wa Tegeta, tayari alishafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Shaidi.

Katika kesi hiyo, inadaiwa, Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, mwaka huo huo, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum katika wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

 Aidha, Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha kiasi cha sh. Milioni nane huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Oktoba 11, mwaka jana majira ya alfajiri katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum mfanyabiashara MO alitekwa nyara na watu wasiojulikana alipokuwa akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...