Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema Serikali ya Tanzania kupitia Benki kuu, imeamua kuweka dhamana kwa kufidia hasara itakayopatikana kwa wanunuzi wa Pamba kwenye soko la Dunia ili waweze kununua Pamba kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kilo.
Akizungumza na Viongozi wa Mkoa na Wakulima kwa nyakati tofauti leo tarehe 15/07/2019 wakati akianza ziara ya siku tatu Mkoani Shinyanga Mhe. Hasunga amesema Serikali imefikia maamuzi hayo katika kikao cha pamoja kati ya Serikali, wanunuzi na baadhi ya wamiliki wa Benki kilichoitishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Mkoani Tabora jana tarehe 14/07/2019.
"Kuanzia leo, Benki kuu itakuwa inakamilisha taratibu zote na wafanyabiashara wataanza kupewa fedha kwa ajili ya kununua pamba" amesema Mhe. Hasunga.
Aidha, amezidi kueleza kuwa, Serikali imezitaka Benki kupunguza riba kutoka asilimia 16 hadi asilimia 11 ili kuwawezesha wanunuzi kupata fedha za kununua pamba.
Hasunga amesema lengo la Serikali ni kuwasaidia wanunuzi waweze kupata fedha ya kununua pamba yote ya wakulima na wakulima wapate fedha kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kilo kama ilivyotangazwa licha ya bei ya soko la Dunia kushuka.
Amewahakikishia wakulima kuwa, vituo vyote kutakuwa na fedha za kutosha kununua pamba na wakulima watapata fedha zao moja kwa moja na pia kuanzia mwaka ujao kutakuwa na mfumo mzuri zaidi wa ununuzi wa pamba usiokuwa na usumbufu kwa wakulima na wanunuzi.
Akielezea changamoto zilizotokana na wanunuzi kushindwa kununua pamba katika msimu huu, Mhe. Hasunga amesema kuwa Serikali ilitangaza bei ya sh. 1,200 kwa kilo baada ya kukokotoa na wanunuzi na kuona bei katika soko la Dunia ipo juu, lakini kutokana na vikwazo mbalimbali bei ya soko la Dunia imeshuka hivyo wakulima watapata hasara iwapo watanunua kwa bei hiyo, pia Benki zilikataa kuwapa fedha kwa kubaini hasara hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amebainisha kuwa, Shinyanga ndiyo Mkoa wenye viwanda vinavyomilikiwa na wazawa ni vema pia kuzungumza na wenye viwanda hivi kufahamu wanahitaji kiasi gani ili waweze kununua pamba inayozalishwa Mkoani hapa. 
Akizungumza na wakulima katika kiwanda cha Afrisian kilichopo Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Telack amewataka wakulima kuhakikisha wanaitunza vizuri pamba ili isishuke ubora wake, kwani pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora na nyuzi zinazofaa kwa kutengeneza nguo.
Mhe. Hasunga yupo Mkoani Shinyanga kwa siku tatu ikiwa ni ziara ya kikazi, pamoja na shughuli nyingine atatembelea vituo vya kununulia pamba.
 Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Shinyanga (hawapo pichani) katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alipoanza ziara yake mchana wa leo
 Msafara wa Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ukiwa katika kiwanda cha Afrisian kuona wakulima wakikusanya pamba yao kwa ajili ya kuuzwa, mbele ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimuongoza Mhe. Hasunga kushuhudia pamba hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akizungumza na wakulima waliokuwepo katika kiwanda cha Afrisian Mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuuza pamba yao  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...