Na Saidina Msangi, WFM, New York, Marekani

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amewasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York nchini Marekani.

Akiwasilisha ripoti hiyo Waziri Mpango ameeleza kuwa Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoamuliwa kutekelezwa na nchi zote ulimwenguni ili kuondokana na umasikini na kuharakisha maendeleo katika nyanja zote.

Akizungumzia lengo namba nne lenye kuangazia elimu jumuishi na bora kwa wote, Dkt. Mpango ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza ambao wana mwaka mmoja wa elimu ya awali kwa asilimia 95.6 mwaka 2018 ambayo ni juu ya makadirio ya asilimia 87.5 ifikapo mwaka 2020.

Aidha, wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kwa asilimia 17.4 ikiwa ni kutokana na mafanikio ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia Dkt. Mpango aliongeza kuwa Tanzania imefanikiwa katika maeneo ya utoaji huduma bora za afya, uongozi bora na amani ya nchi kwa ujumla.

Ripoti hiyo imepokelewa vizuri katika Jukwaa hilo la Umoja wa Mataifa ambapo nchi zilizotoa maoni kuhusu ripoti hiyo ikiwemo Kenya zimepongeza juhudi zilizofikiwa na Tanzania katika utekelezaji wa malengo endelevu.

“Malengo haya ndio dira ya maendeleo na yanaunganika na mipango yetu ya maendeleo kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, na MKUZA kwa upande wa Zanzibar hivyo ni lazima tutekeleze malengo haya kwa bidii,” alisema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa na nchi zenye utaalamu kuisaidia Tanzania katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kufikia azma ya malengo endelevu upande wa utunzaji wa mazingira.

Waziri Mpango amewashukuru wadau wote, sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kwa ushiriki wao katika kuandaa ripoti hiyo kwa kiwango kizuri. Aidha ametoa wito kwa taasisi na sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha na utaalamu zitumike kwa ajili ya kushughulikia utekelezaji wa malengo endelevu. 

Tanzania imeungana na nchi zote duniani katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoazimishwa miaka minne iliyopita ikiwa ni mkakati wa kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Mikutano hiyo yenye kauli mbiu uwezeshaji wa watu na kuhakikisha ujumuishwaji na usawa imekutanisha nchi mbalimbali ambazo zimetuma wawakilishi kutoka Serikalini na Sekta binafsi, inatoa fursa kwa nchi kuweza kutathmini mafanikio, changanoto na mambo ya kujifunza katika kuelekea utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akipongezwa na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez, baada ya kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York nchini Marekani. Katikati ni Mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Modest Mero
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania baada ya kuwasilisha ripoti ya Hiyari ya Utekelezaji wa Malengo Endelevu katika mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri New York nchini Marekani.(Picha na Saidina Msangi, WFM, New York Marekani)
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), akiwasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York nchini Marekani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...