Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpata zawadi muuguzi wa chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutoka shirika la CardioStart International la nchini Marekani Anasi Griffin wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalamu kutoka shirika hilo ambao kwa kushirikiana na JKC wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Shirika la CardioStart International la nchini Marekani wakimfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu kwenye moyo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya siku 14 inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 26 wakiwemo watoto 13 na watu wazima 13 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Daktari wa chumba cha uangalizi maalum kwa watoto kutoka shirika la CardioStart International la nchini Marekani Barbara Ferdman akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalamu kutoka shirika hilo ambao kwa kushirikiana na JKC wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima.(PICHA NA JKCI)

NA MWANDISHI MAALUM

WAGONJWA 26 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya siku 14 inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Waliofanyiwa upasuaji ni watoto 13 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo na valvu kutofanya kazi vizuri na watu wazima 13 ambao wamefanyiwa upasuaji wa kubadilishwa valvu moja hadi tatu ambazo hazikuwa zinafanya kazi vizuri na kupandikizwa mishipa ya damu ya moyo (Coronary artery bypass grafting - CABG).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji Dkt. Anjela Muhozya alisema matibabu hayo yanafanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la CardioStart International la nchini Marekani.

Dkt. Anjela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) alisema katika kambi hiyo walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 40 kati ya hao watoto 20 na watu wazima 20 , hadi sasa wameweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 26 ambao hali zao zinaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kutoka ICU na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuanza mazoezi pamoja na kuendelea na matibabu mengine. 

“Katika watoto tuliowafanyia upasuaji, mtoto mmoja alikuwa na tatizo kubwa la valvu zake tatu kutokufanya kazi vizuri, leo hii tunamfanyia upasuaji na kumwekea valvu nyingine tatu”. 

“Kuwepo kwa kambi hii kumesaidia kwa kiasi kikubwa kwa wagonjwa waliohitaji matibabu ya utaalamu wa hali ya juu kufanyiwa upasuaji wakiwa hapa nyumbani pia kubadilishana ujuzi wa kazi kati yetu na wenyeji kwani katika kambi hizi huwa tunajifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wataalamu wageni ambao wanakuja kufanya kazi na sisi”, alisema Dkt. Anjela.

Kwa upande wake Kasilda Koka ambaye binti wake amefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo aliishukuru Serikali na wafanyakazi wa JKCI kwa kumpokea binti yake na kumfanyia upasuaji huku akitibiwa kwa kutumia bima ya afya.

“Mwaka 1999 wakati huduma za upasuaji wa moyo hazikuwepo hapa nchini nilimpeleka mwanangu ambaye alikuwa na tundu katika moyo kutibiwa nchini India ambako nilitumia gharama kubwa” . 

“Hivi sasa binti yangu alikuwa na shida ya valvu moja kutofanya kazi vizuri ameweza kufanyiwa upasuaji hapa nchini na kuwekewa valvu nyingine kama mnavyomuona anaendelea vizuri”, alisema Kasilda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...