Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

WAZEE wa baraza katika kesi ya mauaji dhidi ya  Yusuph Mussa Mkazi wa Mchikichini, anayedaiwa kumuua mke wake, wameieleza Mahakama kuwa, upande wa mashitaka katika kesi hiyo, wameshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshtakiwa hivyo wanamuona mshitakiwa hana hatia.

Wakitoa maoni yao leo, mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo wazee hao wamedai kati ya mashahidi tisa waliotoa ushahidi  dhidi ya mshitakiwa huyo, hakuna hata shahidi mmoja aliyeeleza kuwa alimuona mshtakiwa akitenda nia hiyo ovu.

Hatua ya wazee hao ambao ni washauri wa mahakama imefikwa baada kufungwa kwa ushahidi wa pande zote mbili pamoja na mawasilisho yaliyofanywa na mawakili kama mshitakiwa ana hatia au la.

Wakitoa maoni hayo, wazee hao wamedai ushahidi wa upande wa mashitaka una mashaka mengi na hauna muunganiko wa matukio yaliyotokea wakati wa kifo cha marehemu Fatuma Mbaga.

Wamedai mashahidi pamoja na mshitakiwa waliieleza mahakama kuwa sababu ya kifo ilidhaniwa imetokana na shoti ya umeme lakini upande wa mashitaka umeshindwa kuwaleta mafundi umeme ili kuthibitisha kama ni kweli nyumba ya mshitakiwa na marehemu ilikuwa na shoti na walirekebisha tatizo hilo kabla ya tukio.

Pia wamedai mahakama haikuletewa tiketi ya ndege aliyosafiria mshitakiwa kwenda Mwanza  kama alivyodai wala tiketi za gari aliyotumia askari mpelelezi kwenda kuchunguza kama baba wa mshitakiwa ni mzima au amekufa pia mpelelezi alishindwa kwenda kwenye kampuni aliyokuwa anafanyia kazi baba wa mshitakiwa ili kuthibitisha kama ni mzima licha ya jitihada za kwenda Mwanza kujua ukweli.

Wameeleza, kuna maswali mengi katika kesi hii kwa sababu daktari alieleza kuwa kifo cha marehemu kilisababishwa na matatizo kwenye ubongo yaliyosababisha kuvuja damu, michubuko sehemu za haja kubwa na ndogo na alivunjika mgongo je yote haya yamesababishwa na hitilafu ya umeme? Amehoji mzee wa baraza.

Kufuatia hayo,  wazee hao wamedai kuwa mshitakiwa hana hatia kwa sababu ushahidi uliotolewa ni wa hisia hivyo,  mahakama imuachie huru.

Mapema, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Robert Kusalika umedai kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka ni wa mazingira na kwamba hakuna mtu aliyemuona mshitakiwa akitenda kosa. Kusalika amedai ushahidi uliotolewa umekata kata hna haumuunganishi moja kwa moja mshitakiwa na tukio hilo.

Aidha Msajili Mazengo amesema ni wajibu wa upande wa mashitaka kuhakikisha wanathibitisha mashitaka bila kuacha shaka na kwamba hakuna shaka kuwa Mbaga alikufa kwani daktari aliyechunguza mwili huo aliithibitishia mahakama na kwamba mshitakiwa na marehemu walikuwa mke na mume ambao waliishi pamoja.

Mussa anadaiwa,  Mei 11 ,2015 eneo la Jangwani ,Ilala, jijini Dar es Salaam, alimuua  kwa makusudi Fatuma Mbaga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...