*Wawili washikiliwa, majina bandia ya moringa na mlonge yatumika kusafirisha madawa hayo

* Kampuni  zinazohusika na usafirishaji wa vifurushi zatakiwa kuchukua tahadhari na kutoa taarifa dhidi ya mizigo itakayotiliwa mashaka

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikiana na shirika la Posta, Wizara ya kilimo na mifugo na Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kukamata zaidi ya kilo 300 za dawa za kulevya aina ya  mirungi iliyokuwa ikiingizwa nchini na kusafirishwa kwenda nchi za Ulaya hasa Uingereza kwa njia ya Posta huku wahusika wakitumia majina bandia ya mlonge, moringa tea, dawa, majani ya mboga, tea leaves na moringa leaves.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamishina wa Intelijensia kutoka Mamlaka hiyo Fredrick Kibuta amesema kuwa baada ya dawa hizo kukamatwa zilipelekwa kwa mkemia Mkuu wa Serikali uchunguzi umethibitisha kuwa majani hayo yana kemikali aina ya Cathinone ambayo inapatikana kwenye mmea wa mirungi (Cath edulis.)

"Taarifa za awali zilibaini kuwepo kwa usafirishwaji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini kwenda nchi za Ulaya kwa njia ya Posta huku shehena hizo zikiwa zimepewa majina bandia, na imebainika  kuwa dawa hizo ziliingizwa nchini kutoka nchini Ethiopia kama majani ya mlonge na baadaye kufungwa upya kusafirishwa tena kwenda Uingereza, Canada, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya" ameeleza Kamishina Kibuta.

Amesema kuwa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiserikali zinaendelea na uchunguzi na kubaini ukubwa wa tatizo ambapo hadi sasa watu wawili wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.


Vilevile amesema kuwa suala hilo haliwahusu wafanyabiashara halali wa zao la mlonge na  waendelee kufanya biashara zao na amezitaka kampuni zinazosafirisha vifurushi kama vile DHL, FEDEX, Swiss Port na wengine kuchukua tahadhari na endapo watapata mashaka yoyote kwenye mizigo hiyo taarifa itolewe haraka kwa mamlaka hiyo.

Kwa upande wake Kamishina wa huduma za sheria Edwin Kakolaki amesema kuwa Serikali ipo macho na yeyote atakayebainika anajihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ile sheria ipo na itafanya kazi yake na kuongeza kwamba kifungo cha maisha gerezani kitamuhusu yeyote atakayekutwa na dawa la kulevya zaidi ya kilo 50 na kifungo cha miaka 30 kwa watakaokutwa na dawa chini ya kilo tajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...