Na Charles James, Michuzi TV

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deo Ndejembi ameagiza Mhandisi wa Wilaya hiyo, Christian Mlay pamoja na mhandisi anaejenga mabweni kwenye Shule ya Sekondari Kongwa kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi.

DC Ndejembi amefikia hatua hiyo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Shule hiyo na kubaini kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha za ujenzi katika Shule hiyo kongwe mkoani Dodoma.

DC Ndejembi amesema ameamua kufanya ziara hiyo baada ya kuona ujenzi wa majengo hayo unaenda taratibu tofauti na mkataba walioingia na mkandarasi huku pia akieleza kutoridhishwa na namna majengo hayo yanavyojengwa.

" Lengo lilikua kukagua maendeleo ya ujenzi huu lakini kama mlivyojionea wenyewe hakuna kitu cha maana kilichofanyika, tulitoa maelekezo kwao cha ajabu hawajayafanyia kazi, mkandarasi anajenga kwa kasi ndogo tena kwa kujisikia, ubora wa majengo ni tofauti na makubaliano tuliyoingia nao, mbaya zaidi kuna ufisadi mkubwa kwenye manunuzi ya vifaa vya ujenzi.

" Mhe Rais anafanya kazi kubwa hizi pesa za ujenzi wa Shule hii kongwe imetoka Serikali Kuu, hatuwezi kuruhusu mambo ya hovyo kufanyika, tumepewa nafasi na Mhe Rais lazima tuwatumikie wananchi kwa uadilifu," amesema DC Ndejembi.

Amesema ujenzi huo unahusisha mabweni mawili, madarasa mawili na bwalo la chakula ambapo kiasi cha Shilingi Milioni 290 lakini mpaka sasa kiasi kilichobaki ni Shilingi Laki moja tu huku mkandarasi akiwa hajamaliza kazi.

Mhe Ndejembi amesema sababu zilizosababisha majengo hayo kutokamilika licha kutengewa fedha nyingi ni kutokana na kutofuata maelekezo ya Serikali ya kutumia Force akaunti ambapo walitangaza tenda hali iliyosababisha ununuzi wa vifaa vya ujenzi kununuliwa kwa bei kubwa tofauti na ilivyo kawaida.

Hivyo Mkuu huyo wa wilaya ameagiza TAKUKURU kufuatilia bei ya Manunuzi

ya Bidhaa hizo za Ujenzi ,milioni 74 zilizobaki kwenye akaunti zisitume mpaka uchunguzi ukamilike na wale wote waliohusika katika ubadhilifu huo wanachukuliwa hatua kwa kumdanganya na kumdharau Rais,Waziri wa TAMISEMI pamoja na yeye.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mjs Deo Ndejembi (kulia) akitoa maelekezo kwa mhandisi wa ujenzi wa bwalo shule ya Sekondari ya Kongwa.
DC Ndejembi akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa madarasa, mabweni katika Shule ya Sekondari Kongwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...