Kama sehemu ya jitihada za kuwanyanyua na kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania wapate ujuzi wa vitendo na kupata ajira kwa urahisi,Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGML) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu,Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu,Taasisi ya Sekta Binafsi(TPSF) pamoja na  Umoja wa Waajiri nchini Tanzania(ATE) wamezindua tena awamu nyingine ya kujenga uwezo na kusaidia  wahitimu wa vyuo vikuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Bw. Richard Jordinson(anayezungumza) akitoa hotuba ya kuzindua mafunzo ya wahitimu wa Vyuo Vikuu kwa mwaka 2019/2020.Kushoto kwake ni Mgeni rasmi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi Janeth Mobe na mwakilishi wa Umoja wa Waajiri nchini Tanzania Bw Danny Sora Tandasi(Kulia)
Mpango huu unawalenga wahitimu wapya kutoka Vyuo Vikuu nchi Tanzania katika taaluma mbalimbali ambao hupewa fursa ya kufanya kazi ndani ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) kwa muda wa mwaka mmoja ili kupata ujuzi wa vitendo husika ambao utawajengea uwezo wa kujiamini  kabla ya kupata ajira rasmi.
Mwakilishi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi Janeth Mobe akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua program ya mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa vyuo Vikuu nchini ambayo inafadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu Geita(GGML)


Akizungumza kuhusu Program hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Bw. Richard Jordinson amesema; “Serikali na Wadau wengine wamekubaliana kuanzisha program hii ya wahitimu wa vyuo vikuu nchi nzima ambayo itatoa fursa kwa wahitimu vijana kupata ujuzi katika maeneo ya kazi ili kuweza kuhusianisha masomo ya darasani pamoja na uzoefu wa vitendo kwenye maeneo ya kazi jambo ambalo ni muhimu sana katika soko la ajira kwa sasa”.

Bw Jordinson alisema kuwa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) ni Kampuni Raia,inayounga mkono jitihada za Serikali kuakisi mitaala inayofundishwa vyuoni pamoja na mahitaji ya ujuzi katika soko la ajira ili kuwasaidia vijana waendelee kuwa na mchango chanya kwenye jamii yao.

“Uhusiano kati ya nadharia na vitendo ni muhimu kwa wahitimu vijana wanapofanya kazi na kushindana katika soko la Ajira. Kupitia Program hii,thamani ya wahitimu vijana katika soko la ajira itaongezeka na kuwa na tija katika safari yao ya ajira ndani ya Mgodi wa Dhahabu Geita(GGML) au kwingineko,”aliongeza Bw Jordinson.


Mwaka jana,Ofisi ya Waziri Mkuu,Ajira,Vijana na Watu wenye ulemavu ilianzisha Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Wahitimu wa Vyuo Vikuu kwa lengo la kuisaidia nchi kufikia kwa urahisi malengo ya uchumi wa pato la kati kama inavyoongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Mwaka 2018/2019, Program ya Mafunzo kwa Wahitimu wa Vyuo Vikuu ndani ya Mgodi wa Dhahabu Geita(GGML) ilitoa ajira 7 kwa wahitimu 22 waliokuwa katika mafunzo hayo.Maeneo yaliyopewa kipaumbele yalikuwa Jiolojia,Uchimbaji,Uchakataji madini,Rasilimali Watu,Sheria,Jamii,Usalama na Mazingira.Faida nyingine ya program hiyo ni kutengeneza idadi ya wahitimu wenye vipawa ili Kampuni inapohitaji wahitimu wenye sifa zinazohitajika iwe rahisi kuwapata nafasi zinapotokea.
“Tunakusudia kuacha alama yenye thamani katika Mji wa Geita pamoja na Tanzania kwa ujumla ambapo kusudio letu ni kuhakikisha uwekezaji wetu wa moja kwa moja kupitia mafunzo hayo tunayoyatoa na ajira tunazotengeneza,tunaendelea kuzalisha mapato na kulipa Kodi zinazohitajika.Tunajivunia sana kuwa sehemu ya wadau wanaofanikisha program hii ili kuleta maendeleo endelevu ya uchumi kutoka kwenye shughuli zetu za uchimbaji dhahabu,” alihitimisha  Bw. Jordinson.
Naye Mwakilishi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi Janeth Mobe aliipongeza GGML kwa kuendeleza program hiyo na kuwataka vijana waitumie fursa hiyo kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
“Mafunzo yenu ni muhimu sana katika kusaidia nia ya serikali kutimiza ndoto ya viwanda na uchumi wa pato la kati,zingatieni kwa umakini mkubwa fursa hii ili iweze kuleta tija na manufaa yaliyokusudiwa hasa kwenye soko la ajira baada ya kumaliza mwaka wenu wa mafunzo kwa vitendo ndani ya Mgodi wa Dhahabu Geita,”alisisitiza Bi Janeth
Kwa upande wake,mnufaika wa program hiyo mwaka huu Bi Diana Ngungi alisema kuwa amefarijika sana kupata fursa ya kupata mafunzo baada ya kuhitimu elimu yake ya Chuo Kikuu.
“Ninayo kila sababu ya kuipongeza GGML kwa kunipatia fursa hii na ninaahidi kuitumia ipasavyo kwa ajili ya kujifunza zaidi kabla sijapata ajira ya kudumu,”alisema Bi Diana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...