Na Ripota Wetu, Michuzi TV

MBUNGE wa Singida Kaskazini Justine Monko amempongeza Rais John Magufuli kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) katika mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo uliomalizika Jumapili Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, Monko amesema hatua ya Rais Magufuli kuteuliwa katika nafasi hiyo ni faraja kwa watanzania wote wakiwemo wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini ambao siku zote wamekuwa wakimuunga mkono kwa juhudi zake za kulileta Taifa maendeleo.

Amesema yeye pamoja na wananchi wa Singida Kaskazini wana imani kubwa na Mwenyekiti huyo mpya wa SADC katika wadhifa wake huo mpya kutokana na kuonesha mafanikio mazuri ya uongozi wake katika Taifa tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa taifa hili katika uchaguzi wa Mwaka 2015.

"Tunaamini ataitendea haki SADC kama ambavyo amekuwa akifanya katika Taifa hili, kwani katika kipindi ambacho amekuwepo madarakani amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo na ujenzi wa uchumi kitu ambacho watu wengi hawakudhani kama kingafanyika, imani hiyo aliyotupa ndiyo tunayoamini kuwa ataiendeleza SADC,"amesema Monko.

Aidha amesema pamoja na kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC, pia mkutano huo wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo ulifana chini ya Uenyeji wake huku hotuba yake ikigusia maeneo muhimu kwa Maendeleo ya Jumuiya hiyo na wananchi wake.

"Jambo hili litazidi kuhimarisha umoja na mshikamano wa nchi hizo kama alivyokuwa ameligusia katika hotuba yake alipokuwa akifunga mkutano huo.Kauli ya Rais Magufuli kusema Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wanachama wa SADC ili kuharakisha jitihada za kuleta maendeleo fungamani, linaonesha ni kwa namna gani ana kiu ya kuziona nchi zote zilizomo ndani ya SADC zinapiga hatua zaidi za kimaendeleo kama alivyo na kiu hiyo kwa Tanzania,"amesema.

Amefafanua kimsingi mambo mengi ambayo Rais Magufuli amegusia katika hotuba yake hiyo yana akisi yale anayoendelea kuyafanya hapa nchini ambayo kwa kiasi kikubwa matokeo yake yanaonekana kwa kadri siku zinavyozidi.

Ametoa rai kwa nchi za SADC kuyatekeleza ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa na kuongez hatua ya Rais Magufuli kuzitaka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuweka mkazo katika usimamizi wa rasimali zake una maana kubwa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Kuhusu lugha ya Kiswahili kuchaguliwa kuwa miongoni lugha ya nne za kutumika katika mikutano ya SADC, Mbunge huyo amesema kunaleta fahari kwa Tanzania kwa kuwa itazidi kulitangaza nchi yetu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...