Na Ripota Wetu,Michuzi TV

WAKATI Rais Dkt  John  Magufuli akielekea kupokea Uenyekiti wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk.Agnes Kijazi amekabidhiwa Uenyekiti wa Kamati ndogo ya Sekta ya hali ya hewa ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha Dk.Kijazi amechaguliwa bila kupingwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “SADC Meteorological Association of Southern Africa (SADC-MASA)” kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2019.  

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari nchini imeeleza kuwa Wilbert Timiza Muruke  ambaye amemwakilisha Dkt. Kijazi amekabidhiwa nafasi hizo katika mikutano ya SADC-SCOM na SADC-MASA iliyofanyika kwa kufuatana jijini Windhoek, Namibia kuanzia Agosti 5 hadi 9 Agosti, 2019. 
 
Imefafanua kuwa  Kama ilivyo kawaida baada ya Rais Dkt. John Magufuli kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC, Sekta zingine zote zinakuwa chini ya uenyekiti wa Tanzania, hivyo kwa upande wa Sekta ya hali ya hewa, tayari TMA imekwishakabidhiwa Uenyekiti wa kamati hiyo ya SADC Sekta ya hali ya hewa (SADC SCOM) kutoka kwa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Namibia.

 Aidha, Uenyekiti wa Tanzania kuongoza umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za SADC (SADC MASA) utadumu kwa miaka miwili, ambapo Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya hali ya hewa ya Lesotho amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC MASA. 

Kabla ya kupokea nafasi hiyo ya kuwa Mwenyekiti wa MASA, Dkt. Kijazi alikuwa Makamu Mwenyekiti na  Franz Uirab kutoka Namibia alikuwa Mwenyekiti.

Akipokea dhamana hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Meneja wa Uhusiano wa Hali ya Hewa Kimataifa, Wilbert Timiza Muruke ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika mikutano hiyo, alishukuru kwa nafasi hizo na kumpongeza aliyekuwa Mwenyekiti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...