Shirika la Kimataifa la Kuhudumia watoto la Save The Children kupitia mradi wake wa Lishe Endelevu unaolenga kuimarisha hali ya lishe kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, wajawazito na wanaonyonyesha, vijana wa rika la balehe na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano limeadhimisha wiki ya Unyonyeshaji duniani mkoani Dodoma.

Kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani yaliyoandaliwa na shirika la Save The Children yamefanyika leo Agosti 7,2019 katika kijiji cha Kingale wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma. 

Meneja wa Shirika la Save The Children Mkoa wa Dodoma Benety Malima alisema maadhimisho hayo ya wiki ya unyonyeshaji ni sehemu ya utekelezaji wa mradi Lishe Endelevu unaofadhiliwa na Mfuko wa Watu wa Marekani 'USAID'.

Malima alitumia fursa hiyo kuwahimiza waajiri kwenye mashirika na taasisi mbalimbali kutenga chumba maalumu kwa ajili ya akina mama kuwanyonyesha watoto wao. Alisema siku 1000 za lishe ya mtoto zinaanzia tumboni na na kuwasisitiza akina mama wajawazito kula vyakula vyenye lishe kabla na baada ya kujifungua. Malima alisema kwa mujibu wa takwimu za hali ya lishe kutoka taasisi ya chakula na lishe kuwa katika mikoa minne ya Dodoma, Rukwa, Iringa na Morogoro ambako shirika lao linafanya nao kazi hali ya lishe hairidhishi. Malima aliwasisitiza wanaume kushirikiana na akina mama katika suala zima la kunyonyesha na kuongeza kuwa wakati mwingine wa baba ni chanzo wa mama kutopata maziwa kutokana na ugomvi hivyo ni vyema wanaume wakawapenda wake wao. 

Aidha alisema lishe kwa wanawake wajawazito inachochea hatari ya kujifungua watoto njiti , waliodumaa au kuharibu mimba. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa alisema takwimu za hali ya ulishaji watoto wachanga na wadogo katika mkoa wa Dodoma takribani asilimia 97 ya watoto wenye umri wa miaka miwili,wananyonyeshwa maziwa ya mama, idadi ya watoto wanaoanzishiwa maziwa ya mama kwa wakati sahihi katika kipindi sahihi kisichozidi saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 57. 

"Idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 47.7, idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6-23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo cha ubora kiliishe ni asilimia 35.9 na idadi ta watoto wanaoanzishiwa vyakula cha nyongeza kwa wakati sahihi katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 85.7,'' alieleza. 

Alibanisha kuwa changamoto ya matumizi ya chumvi yenye madini joto, ni asilimia 81 ndio wanatumia chumvi yenye madini joto la kutosha, mama mjamzito anatumia chumvi siyo na madini joto, hivyo afya ya mtoto inaathiriwa sana kwani anaweza kuzaliwa akiwa na udumavu wa ubongo au ulemavu wa viungo. 

''Nitoe rai kwa wazazi na walezi kutafuta taarifa sahihi kuhusu unyonyeshaji unaofaa kutoka kwa mtoa huduma ya kiafya katika jamii, mtaalam wa afya kipindi cha ujauzito hili likienda sambamba na kuhudhuria kliniki mapema pindi tu mama anapojigundua ni mjamzito,'' alisema Mkurugenzi huyo. 

Aliwataka akina baba kuwasindikiza wenza wao kliniki ili kuhakikisha kwamba mume/mwenza na familia wana taarifa kuhusu malengo ya unyonyshaji ili waweze kutoa msaada , pia aliwasisitiza kina mama wanaonyonyesha kuainisha msaada wa vitendo unaohitajika na kuomba msaada kutoka kwa mume/mwenza, familia na ndugu wengine ili kupata msaada. 

Nao baadhi ya akina mama waliohudhuria katika maadhimisho hayo akiwemo Sikitu Damian Lyimo aliwataka akina mama wote nchini kula vyakula vyenye lishe ili kuweza kuzaa watoto wenye afya njema na akili timamu. Aliongeza kuwa wamepata elimu ya kutosha Shirika la Save the Children hivyo watahakikisha wanaitumia ipasavyo kwa kuwa vyakula vyote vyenye lishe bora vinapatikana kijijini hapo. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani leo Agosti 7,2019 katika kijiji cha Kingale wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma. 
Meneja wa Shirika la Save The Children Mkoa wa Dodoma Benety Malima (mwenye tisheti nyekundu kulia) akiwa kwenye Kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani yaliyoandaliwa na shirika la Save The Children leo Agosti 7,2019 katika kijiji cha Kingale wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma. 
Zoezi la upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wa miezi 6 hadi 59 likiendelea. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa akishuhudia mafunzo ya upishi wa chakula cha watoto kwa wanajamii hususani akina mama. 
Kulia ni Mtaalamu wa afya akionesha aina mbalimbali za za vyakula lishe vinavyopatikana katika mkoa wa Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...