Na Ales Mbilinyi - JKCI

23/08/2019 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeiahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inatoa elimu kwa wataalamu wa magonjwa ya moyo waliopo Hospitali ya Mnazi mmoja ili wananchi wanaotibiwa katika Hospitali hiyo wapate huduma za kisasa na za utaalamu wa hali ya juu .

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alipokutana na wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa.

Prof. Janabi alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipokea wataalamu kutoka Hospitali mbalimbali hapa nchini zikiwemo za Benjamini Mkapa, Bugando na KCMC ambao walijifunza jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo kwa njia za kisasa na utaalamu wa hali ya juu na baaada ya kumaliza mafunzo yao walikwenda kuyafanyia kazi katika maeneo yao waliyotoka kitu ambacho kimesaidia wananchi kupata matibabu ya moyo yanayoendana na wakati uliopo.

“Umefika wakati sasa uzoefu walionao wataalamu wa afya wa JKCI ukatumika kuwafundisha wataalamu wengine wa afya wakiwemo wa kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja. Kama mtakuwa tayari watumeni wataalamu wenu waje kujifunza kwetu japo kwa kipindi cha miezi mitatu nasi tutawafundisha utaalamu wote tulionao”.

“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iko tayari kushirikiana na Hospitali ya Mnazi mmoja kwa kutuma wataalamu wake na kufanya matibabu ya pamoja kwa wagonjwa wa moyo wanaotiiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja”, alisema Prof. Janabi.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema tangu kusainiwa kwa mkataba wa kupokea wagonjwa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya wagonjwa 26 wameshatibiwa katika Taasisi hiyo na hali zao zinaendelea vizuri.

“Baada ya kusaini mkataba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwishoni mwa mwaka jana tulianza kuwapokea wagonjwa wa moyo kutoka Zanzibar. Hadi sasa wagonjwa 26 wamepata matibabu ya upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na bila kufungua kifua, miaka ya nyuma wagonjwa hawa walikuwa wanapelekwa nje ya nchi lakini hivi sasa wanatibiwa hapa nchini na wataalamu wetu”, alisisitiza Prof. Janabi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo mwenyekiti wa kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Mhe. Mwanaasha Juma amesema kupitia ziara waliyoifanya katika Taasisi hiyo wameweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia katika kuhakikisha huduma bora za matibabu ya moyo zinapatikana Zanzibar.

“Ujio wetu hapa utatuwezesha kuendelea kutoa rufaa kwa wagonjwa wa moyo walipo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuja kutibiwa hapa JKCI badala ya kuwapeleka nje ya nchi kupatiwa matibabu ambayo yanapatikana hapa hapa Tanzania. Kama kamati tumeridhika na huduma zinazotolewa kwani tumejionea kwa macho yetu na ni furaha kuwa wagonjwa wetu kutibiwa katika nchi yao kwa mazingira waliyoyazoea,” alisema Mhe. Mwanaasha

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman aliishukuru Taasisi hiyo kwa mapokezi mazuri waliyowapatia na kuahidi wataendelea kushirikiana zaidi katika kuhakikisha wananchi wanapata matibabu mazuri ili watoke hapo walipo na kusonga mbele zaidi katika huduma za matibabu ya moyo.

Mhe. Harusi aliuomba uongozi wa JKCI kuwapeleka mara kwa mara wataalamu wake katika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kufanya matibabu ya pamoja bila kuchoka ili mafunzo yatakayotolewa yawe na tija kwa wataalamu hao na kwa wananchi waweze kupata matibabu ya kibingwa.
 Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya  Kikwete (JKCI) wa wodi ya  watoto Theresia Tarimo akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jinsi wanavyowahudumia watoto wanaolazwa katika wodi hiyo.  Kushoto kwa Theresia ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman ambaye aliambatana na wajumbe hao ili kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo. 
 Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa chumba cha Cathlab Rogers Kibula akiwaelezea wajumbe wa kamati ya Ustawi wa Jamiii ya baraza la wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  jinsi upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua pamoja na uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo unavyofanyika katika kwa kutumia mtamo wa  Cathlab wakati wa ziara ya wajume wa baraza hilo ya kuona huduma  mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi, Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wafanyakazi wa JKCI mara  baada ya wajumbe hao kumaliza ziara yao ya kutembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Picha na JKCI

 Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yao ya kuangalia huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...