Kamishina wa walipakodi wakubwa wa Mamlaka ya mapatoTanzania (TRA), Alfred Mregi akizungumza katika semina ya kutoa elimu ya kodi kwa
 wafanyakazi wa taasisi na mashirika ya umma katika ukumbi wa mikutano, benki kuu jijini Dar es Salaam leo. Akimwakilisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dr. Edwin Mhede.
 Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Herbert Kabyemela akizungumza na wawakilishi wa taasisi na mashirika ya umma wakati wa kutoa elimu katika ukumbi wa mikutano, Benki kuu jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wawakilishi  wa taasisi na mashirika ya umma wakimsikiliza Kamishna wa walipakodi wakubwa wa Mamlaka ya mapatoTanzania (TRA), Alfred Mregi katika ukumbi wa mikutano, benki kuu jijini Dar es Salaam leo wakati wakipewa elimu TRA kuhusiana na kujifunza namna kutumia mifumo mipya ya kukusanyaji kodi nchini. 
Kamishna wa walipakodi wakubwa wa Mamlaka ya mapatoTanzania (TRA), Alfred Mregi na Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Herbert Kabyemela wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi na mashirika ya umma katika ukumbi wa mikutano, Benki kuu jijini Dar es Salaam leo.Picha na Avila Kakingo, Michuzi Blog

Na Karama Kenyunko, blog ya jamii.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), amezitaja changamoto ambayo  taasisi na mashirika ya umma zimekuwa zikikabiliana nazo ikiwemo kushindwa kuwasilisha ritani na kushindwa kuwasilisha mapema.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina  iliyohusisha Wahasibu wa Taasisi mbalimbali za umma , Kamishna wa Idara ya Walipakodi wakubwa, Alfred Mregi kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, amesema,  kuwa taasisi hizo zimekuwa zikifanya manunuzi au matumizi yasiyokuwa na stakabadhi au Ankara za kodi za kielektroniki.

Pia ameongeza kuwa, taasisi hizo zimekuwa na madeni makubwa ya kodi ya muda mrefu na wamekuwa wakikosea katika kufanya malipo ya kodi mbalimbali mara kwa mara kwenye mfumo wa malipo wa kodi na maduhuli.

‘’Bado kuna changamoto au mapungufu katika tafsiri na ukokotoaji wa kodi kwenye mishahara, posho na stahiki mbali mbali za watumishi, vibarua na makandarasi hususani kwenye miradi mbali mbali,’’ amesema Dk Mregi..

Ameongeza kuwa yapo mapungufu katika tafsiri na utozaji wa kodi ya zuio hususani katika kandarasi, miradi na zabuni mbali mbali na kutokuzingatia matumizi sahihi ya mabadiliko mbali mbali yatokanayo na sheria za fedha za miaka husika, hivyo kusababisha taasisi na mashirika husika kukadiriwa ongezeko la kodi, adhabu na riba. 

Mregi amesema lengo la kuwataka wananchi kulipa kodi litatimia endapo watashirikiana kutimiza wajibu ikiwemo kulipa kodi stahiki kwa wakati, kuboresha ushirikiano baina ya serikali na wafanyabiashara, kutofumbia macho vitendo vya rushwa, uhalifu na uhujumu uchumi na vitendo vingine ambavyo vinasababisha nchi kupoteza mapato.

‘’Mamlaka ya mapato inaendelea kushirikiana na wadau wake ili kuongeza uelewa wa sheria na taratibu mbalimbali na kuongeza uhiari katika ulipaji kodi,’’ amesisitiza.

 Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza, ujuzi, elimu na weledi wa matumizi bora ya mifumo ya kodi kwani TRA ina wajibu wa kusimamia sheria mbalimbali za kodi pamoja na maduhuli kwa niaba ya serikali na ina mkataba wa huduma kwa mlipa kodi na kwamba dhamira yake ni kutoa huduma bora kwa walipakodi na wadau wengine katika utekelezaji wa majukumu yake kisheria.

Naye Naibu Kamishna wa Idara ya walipakodi wakubwa Herbert Kabyemela amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2019/20 mamlaka ya mapato inajukumu la kukusanya Sh trilioni 19.1 ikiwa ni asilimia 57.6 ya Bajeti ya serikali ya Sh trilioni 33.11.

Amesema lengo hilo ni sawa na ongezeko la Sh trilioni 1.1 ukilinganisha na lengo la mwaka wa fedha wa 2018/19 

Kwa upande wake Dinna Zacharia ambaye ni muhasibu kutoka Shirika la 
 Mawasiliano Tanzania (TTCL) alisema kuwa semina hiyo itawasaidia 
walipakodi kujua mifumo ya kodi iliyopo lakini pia aina za kodi 
wanazotakiwa kulipa.

Amesema pia itawawezesha kujua mabadiliko ya shera za kodi yaliyojitokeza  na kuweza kuyafanyia kazi na hatimae kuiwezesha serikali kutimiza lengo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...