*Vyombo vya moto 126 vyakamatwa kwa kukiuka sheria elekezi zipo pikipiki, bajaji na magari yenye ving'ora na taa sumbufu

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetangaza kuanza kutumia helkopta kwa ajili ya kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha wageni wote waliopo na watakaoingia nchini wanakuwa salama katika kipindi chote cha mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC).

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya  Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema wageni wanazidi kuja nchini na jeshi hilo lipo makini kuhakikisha hakuna aina yoyote ya uvunjifu wa amani utakaotokea.

"Msako na doria wa askari watumiao magari, pikipiki, mbwa, farasi, na watembeao kwa miguu unaendelea katika sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam na kuanzia kesho helkopta itatumika katika kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya Dar es Salaam" amesema


Kamanda Mambosasa amesema baada ya kuzuia pikipiki, magari yenye ving'ora na gari  zenye taa sumbufu na bajaji kutoingia katikati ya mji,bado kuna watu wameendelea kukiuka agizo hilo ambapo hadi sasa jumla ya vyombo vya moto 126 vimekamatwa na vinashikiliwa na jeshi la polisi.

"Tuliweka zuio la baadhi ya vyombo vya moto kutoingia katikati ya mji katika kipindi hiki cha mikutano ya SADC ,  kuna baadhi wamekiuka hasa pikipiki (bodaboda) ambazo zimekuwa hazifuati sheria, wanabeba mishikikaki, hawavai kofia ngumu na kupitia msako uliofanywa na jeshi la polisi vyombo vya moto 126 vimekamatwa na hivyo vikihusisha pikipiki 87, bajaji 13 na magari yenye ving'ora na taa sumbufu barabarani 26 na baadhi ya wahusika wanashikiliwa na watapelekwa mahakamani" ameeleza Mambosasa.

Pia amewahakikishia wananchi na wageni usalama wa hali ya juu na bado wanaendelea na kazi ya kuhakikisha jiji hilo linaendelea kubaki salama salimini hata baada ya mkutano huo kumalizika

"Jiji lipo shwari kabisa tulikuwa na uhaba wa askari polisi 300 lakini tumeongezewa wengine wengi , hivyo msako utaendelea na watakaojaribu kukaidi kile kinachoelekezwa na Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi  na usalama watakutana na vyombo vya dola na ninazidi kuwahimiza wananchi kuunga mkono jeshi la polisi hasa kwa kutoa taarifa za uharifu na waharifu kwa kuwa mafanikio yatakayotokana na mkutano huo ni yetu sote" ameeleza.
Ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda, wakuu wa Wilaya, madiwani, wenyeviti wa mitaa, vyama vya ulinzi shirikishi na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wanaoonesha hasa katika kipindi hicho ambacho taifa linategemea kuupokea ugeni mzito kutoka mataifa 15.

Kuhusu watakaoendelea kukaidi na kundelea kufanya usumbufu jeshi hilo litaendelea kuwachukulia hatua na kuongeza mkaidi hafaidi mpaka siku ya idi. "Na Idi imeshapita, hivyo tutaendelea kushughulika na hao ambao watakaidi,"amesema Mambosasa.
Kamanda Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari za SADC,kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo,kuhusu namna Jeshi la Polisi lilivyojipanga katika kuhakikisha wageni wote watakaoingia nchini wanakuwa salama katika kipindi chote watakachokuwa nchini .Picha na Michuzi JR.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...