Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Zoezi la kupata dhamana kwa aliyekuwa rais wa club ya Simba Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange Kaburu limegonga mwamba kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuondoa mashtaka ya utakatishaji fedha katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Hatua hiyo imekuja wakati washtakiwa hao walipopandishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama hiyo kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana ili waweze kuachiwa huru.
Na kujiteteaa

Mapema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Wakili kutoka Takukuru, Leornad Swai amedai, kuwa DPP amewasilisha kusudio la kukata rufaa kutokana na uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa jana wa kuyaondoa mashtaka mawili ya utakatishaji baada ya mahakama kuona kuwa hawana kesi ya kujibu kwenye mashtaka hayo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Nehemia Nkoko ameomba mahakama zoezi la kuwapatia dhamana wateja wake liendelee kwani upande wa mashtaka jana walipoulizwa kama wanapingamizi lolote juu ya washtakiwa kupewa dhamana baada ya kuondolewa mashtaka hayo ya utakatishaji, walisema hawana pingamizi lolote.

Amesema,  hoja za serikali zinasimamia katika mashtaka hayo mawili yaliyoondolewa ya utakatishaji na kwamba hawajaweka kusudio la kupinga dhamana.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amesema sheria inawapa nafasi upande wa mashtaka kusikilizwa na kupeleka maombi yao, hivyo ameahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu (Septemba 23) mwaka huu.

Washtakiwa Kaburu na Aveva wamerudishwa rumande.

Jana mchana, Mahakama hiyo iliondoa mashtaka mawili kati ya tisa yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao kwa kuonekana kuwa hawana kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo dhidi yao.

Hata hivyo, washtakiwa hao pamoja na mwenzao Zacharia Hansppope walikutwa na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa

Kufuatia kuondolewa kwa shtaka hayo ya utakatishaji  washtakiwa walipewa masharti ya dhamana ambayo walitegemea kuyakamilisha leo.


Katika uamuzi ulisomwa mahakamani hapo, Hakimu Simba  amesema ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha mashtaka yote kwa washitakiwa na kila shtaka linatakiwa kuthibitishwa peke yake na sio kwa kutegemeana.

 "Baada ya kuchambua ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashitaka, ukiacha shtaka la tano na sita mahakama imeona kuwa washtakiwa wanakesi ya kujibu katika shtaka la 1,2,3,4,7,8 na 9  isipokuwa katika shitaka la tano na sita na  ambayo shtaka la utakatishaji linaondolewa" amesema hakimu Simba.

Kufuatia kuondolewa kwa mashtaka hayo, Wakili wa washtakiwa hao Nehwmia Nkoko ameomba mahakama kuwapatia wateja wake dhamana kwani mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliyokuwa yanawanyima dhamana washitakiwa hayapo.

Wakili wa Takukuru, Leornad Swai alipoulizwa kama anapingamizi lolote juu ya dhamana alidai hawana pingamizi ambapo Hakimu Simba aliwapatia masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini 2 watakaosaini bondi ya Sh.Mil 30 kwa kila mmoja pamoja na kuwa na vitambulisho.

Katika shtaka la kwanza,  Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Katika shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Katika shtaka la tatu Aveva na Kaburu  wanadaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Pia Katika shtaka la nne Aveva anadaiwa katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa USD 300,000

Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia USD 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.

Aveva, Kaburu na Hans Poppe  wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya USD 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577

Shtaka la tisa, Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...