Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ntinko, Editha Mtinda akichangia hoja katika Bunge la Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilaya Singida Vijijini lililofanyika mjini Singida juzi.
Majadiliano yakiendelea.


Na Dotto Mwaibale, Singida

BUNGE la Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wila ya Singida Vijijini limeibua changamoto zinazotakiwa kufikiwa na Serikali kupitia bajeti yake ya kila mwaka.

Changamoto hizo zilibainishwa mwishoni mwa wiki wakati wa majadiliano ndani ya bunge hilo liliketi kwa siku tatu mjini Singida ambalo liliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Mtinko Education Development Organization (MEDO) kwa ufadhili wa Shirika la Norad kupitia ActionAid.

Akichangia hoja katika Bunge hilo lililowakilishwa na wanafunzi 40 kutoka katika halmashauri hiyo Editha Mtinda ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ntinko alisema katika maeneo ya vijiji yenye watu wengi miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikisuasua kutokana na bajeti inayotengwa kuwa ndogo na kutofika kwa kiasi kinachotakiwa.

"Bajeti inapotengwa kwenda katika maeneo hayo haifiki kama inavyotakiwa hivyo kusababisha miradi mingi ya maendeleo kama ujenzi wa shule, zahanati na miradi mingine kushindwa kukamilika" alisema Mtinda.

Mratibu wa Miradi wa Shirika hilo Iddy Mruma alisema walianzisha bunge hilo la wanafunzi ili waweze kuibua changamoto zilizopo katika maeneo wanayoishi na kuzionesha kwa serikali ili zifanyiwe kazi.

Alisema shirika hilo limekuwa likihimiza jamii kujenga tabia ya kulipa kodi itakayosaidia kuongeza ukubwa wa bajeti ya serikali pamoja na kuanzishwa kwa miradi inayopaswa kuhojiwa na kusimamiwa na jamii.

"Jamii inapaswa kuwa na uwezo wa kuhoji miradi yote inayofanywa na serikali katika maeneo yao pamoja na kuisimamia" alisema Mruma.

Alisema bajeti inapotengwa inatakiwa kutoa kipaumbele kwa makundi kama ya wanawake na walemavu kutokana na makundi hayo kusahaulika mara kwa mara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...