Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

RAIS mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu ambayo itawasaidia na kuwafaa kwa baadaye, na ili kufanikisha hilo lazima kuwe na  ubunifu pamoja na kuboresha mitaala ya elimu ambayo itawaongoza kuyafikia malengo yao.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 16 ya shule ya msingi Hekima Waldorf iliyopo Goba Kinzudi Kikwete amesema kuwa elimu inayotolewa lazima ijibu mahitaji ya ajira na elimu inayotolewa kwa kizazi  cha sasa lazima iendane na soko la dunia kwa wakati huu na hata miaka 50 ijayo na hiyo ni pamoja na kuboresha mitaala itakayowaongoza vijana katika kutimiza ndoto zao.

Kikwete amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa jinsi maendeleo ya sayansi na teknolojia yanavyozidi kukua ndivyo waliopambana kusoma watakavyonufaika.

"Wekeni malengo yenu mbele na piganieni ndoto zenu ili muweze kuyafikia malengo yenu, na ninawapongeza wazazi kwa juhudi wanazoonesha katika kuhakikisha mnapata elimu bora kabisa, pamoja na uongozi wa shule ambao daima umehakikisha mnapata maarifa tosha na yenye tija" ameeleza Kikwete.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mzengi amesema kuwa elimu inayotolewa na shule hiyo ni ile inayoendana na mazingira halisi yanayoendana na soko la ajira, na hiyo ni pamoja na kuwafundisha wanafunzi maadili na tabia njema.

Mzengi amesema kuwa ushirikiano uliopo baina ya walimu, wanafunzi pamoja na wazazi umekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha kukidhi malengo ya kielimu. Pia ameishukuru serikali na Wizara ya elimu kwa kutambua ubora na utofauti wanaouonesha katika kuwafundisha watoto kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa elimu hiyo ya kiwaldorf imesambaa katika nchi zaidi ya 120 duniani na kinachowavutia wengi ni namna watoto wanavyolelewa na kufunzwa kwa kuzingatia akili, fikra, utashi na nguvu ya kutenda kwa weledi.

Awali alisoma historia ya shule hiyo Mwalimu. Stephen Chambo amesema kuwa kuanza kwa elimu ya Kiwaldorf mwaka 1997 ulipokelewa vizuri na viongozi pamoja na wadau wa serikali hapa nchini na Hekima imekuwa shule pekee ambayo imekuwa na utaratibu wa kuwaendeleza walimu pamoja na wafanyakazi sambamba na kuandaa warsha na makongamano mbalimbali ya kielimu.

Amesema kuwa daima wamekuwa wakizingatia kauli mbiu yao ya "Learning With Love" ambayo inaendelea kujenga hamasa ya kujifunza na kudumisha upendo wa kweli katika utoaji elimu na malezi, na amewahakikishia wazazi kuwa wanafunzi wanaotoka katika shule hiyo wameiva kielimu na kimalezi na hivyo kuwa waadilifu kiasi cha kutambulika kwa urahisi katika kundi la watoto.
 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akisoma hotuba yake leo katika mahafali ya 16 ya shule ya msingi Hekima Waldorf iliyopo Goba Kinzudi wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,ambapo aliupongeza uongozi wa shule hiyo  kwa kazi nzuri ya kuelimisha watoto. 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kikabidhi vyeti  kwa mwanafunzi  wakati wa Mahafali ya 16 ya darasa la saba ya shule ya msingi Hekima Waldorf iliyopo Goba Kinzudi wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya Msingi Hekima Waldorf,Augustino  Mbogella akisoma historia fupi ya shule hiyo.


 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa shule ya Hekima Waldorf  na baadhi ya wageni waalikwa mwishoni wa shughuli za mahafali hayo.

(Picha zote na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...