Na Karama Kenyunjo, Michuzi Tv.

MWANDISHI wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera anayekabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, matibabu aliyopatiwa na madaktari wa Gereza la Segerea  ya kumpima damu na kumchoma sindano tatu kutokana na kushindwa kupumua na mguu mmoja kukosa nguvu bado hayajatosheleza.

Amedai kuwa,  anapata maumivu makali katika mguu wa kulia na mfupa wa paja  na kumfanya ashindwe kutembea na kusababisha kuburuza mguu lakini bado hajapata huduma nyingine.

Mshtakiwa Kabendera amedai hayo leo Septemba 12, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile  baada ya kutakiwa kueleza kama madaktari wamempatia tiba yoyote.

Amedai madaktari wa gerezani hawana vifaa vya kuwasaidia kugundua tatizo linalomkabili, hivyo wamemshauri kufanya mazoezi lakini amedai mguu wake wa kulia na mfupa wa paja wa mguu huo una maumivu makali 

"Nimefanya jitihada za kuzungumza na madaktari na niliomba dawa za kutuliza maumivu kwa sababu sipati usingizi lakini Madaktari wameahidi kuendelea kuniangalia, na akaongeza kudai kuwa, alionana na daktari Alhamis iliyopita na jana  lakini hakumfanyia vipimo kwa sababu walikuwa na wageni, hivyo aliahidi kuonana naye leo.

"Nipo Segerea na kuna utaratibu wa madaktari kufanya matibabu kwa wagonjwa kila siku," alidai.

 Kabendera ameeleza hayo kufuatia Wakili wake, Jebra Kambole kudai kuwa hali ya mshitakiwa huyo inazidi kutetereka kwa sababu anashindwa kutembea vizuri na kushindwa kupumua.

Kambole amedai mteja wake hajafanyiwa matibabu vizuri kujua tatizo linalomsumbua na kuomba mahakama ielekeze magereza wampeleke hospitali yoyote ya Serikali ikiwamo Muhimbili ili wapate ripoti ya ugonjwa unaomsumbua.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Wankyo Simon amedai amewasiliana na Mkuu wa Gereza na amemueleza kuwa Kabendera anapatiwa matibabu na madaktari wamekuwa wakimuangalia mara kwa mara.

Amedai magereza wana utaratibu  wao endapo wataona ugonjwa unaomsumbua unahitaji rufaa, watampeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu na kumuelekeza Kabendera kuonana na daktari na kesi itakapotajwa ataieleza mahakama kama amepata matibabu au la ili mahakama itoe maelekezo.

Kabendera alifikishwa  Mahakamani kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la Uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh. 173.2Milioni.

Anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es, Salaam, mshtakiwa Kabendera alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Inadaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa  bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya sh. 173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Inadaiwa  kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha sh. Milioni 173.2 wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...